Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian amewataka maafisa tarafa na watendaji wa kata kusimamia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuhakikisha Halmashauri inakusanya mapato ya kutosha. Ameyasema hayo alipokuwa akihutubia kwenye ufungaji wa mafunzo ya kuwajengea uwezo maafisa tarafa na watendaji wa kata uliofanyika katika ukumbi wa Isike Mwanakiyungi, Manispaa ya Tabora Novemba 27, 2023.
“kutokana na mafanikio na maarifa mliopata katika mafunzo haya, nawaagiza kuendelea kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato na matumizi kwa kushirikiana na viongozi wa ngazi ya kata na vijiji” alieleza Mkuu wa Mkoa.
Sambamba na hilo, Mkuu wa Mkoa amewahasa maafisa tarafa na watendaji kushughurikia kero na malalamiko ya wananchi ili kuhakikisha changamoto zinatatuliwa kwa kuanzia ngazi ya kata na vijiji hususani migogoro ya ardhi ambayo kila kukicha imeongezeka kwenye jamii zetu.
“Ninapenda kuwahasa kuwa tatueni kero na malalamiko ya wananchi katika maeneo yenu, jengeni na endelezeni mahusiano mazuri kati yenu na wananchi ili kuelewa changamoto zilizopo hususani changamoto ya migogoro ya ardhi ambayo kila siku inaibuka katika jamii zetu na migogoro mingi inaanzia huko kwenye kata na vijiji” aliongeza Mhe. Batilda
Aidha, Mhe. Batilda amewataka maafisa tarafa na watendaji wa kata kuhimarisha suala la usalama, amani na utulivu kwenye maeneo ya kata na vijiji ili kuhakikisha Serikali inatimiza malengo yake ya kuhimarisha usalama, amani na utulivu.
“Kama mnavvyojua jukumu la msingi la Serikali ni kuhakikisha usalama, amani na utulivu vinakuwepo kwenye maeneo yenu wakati wote, na hivyo hakikisheni mnawashirikisha wananchi kikamilifu kwa kujenga mahusiano mazuri ili kusaidia kutoa taarifa kwenu na vyombo vya ulinzi na usalama kwenye maeneo yenu” alisisitiza Mhe. Batilda
Kwenye mafunzo hayo jumla ya Makatibu Tarafa 22 na Watendaji wa kata 206 kutoka Wilaya saba za Mkoa wa Tabora walifaidika na mafunzo ya kukuza utendaji kazi yaliofanyika katika Ukumbi wa Isike Mwanakiyungi.
Mafunzo hayo yalifunguliwa na Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya Novemba 26, 2023 na kufungwa Novemba 27, 2023 na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa