Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe ameahidi kuunga mkono muunganiko wa mashirika yanayohusika katika utoaji wa huduma za bima za Mazao kwa wakulima ili kuhakikisha majanga ya asili yanakabiliwa kikamilifu. Akizindua Muunganiko wa Mashirika ya Bima (Konsotia) Julai 1, 2023, Waziri Hussein Bashe amesema kuwa “Serikali itaangalia namna ya kuunga mkono muunganiko huo kwa kuweka kiasi cha fedha ili kuongeza nguvu na kuvutia wadau wengine”
Aidha, Mhe. Bashe ameutaka muunganiko huo kupanua wigo wa huduma zake kwa kuhakikisha majanga yote yanayowakumba wakulima yanapata ufumbuzi hasa mabadiliko ya bei wakati wa masoko “Ni hatua nzuri kuhudumia wakulima pale wanapopata majanga kama ukame na mvua za mawe lakini muende mbele zaidi kuangalia mabadiliko ya bei katika masoko” Aliseme Mhe.Bashe.
Kwa upande wa Kamishina wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima (TIRA), Dkt,. Baghayo Saqware ameeleza kuwa muunganiko huo utasaidia wakulima wengi pindi majanga yatakapotokea. Na kwamba muunganiko huo umekusanya mtaji wa kutosha kutoka kwenye mashirika mbalimbali ili kuwafikia wakulima wengi nchini kote.
Naye Ndugu. Elia Kajiba Mtendaji wa Umoja wa Mashirika ya Bima amemuhakikishia Waziri wa Kilimo kuwa, gharama za kulipia bima ya Mazao zitaangalia vigezo maalumu kulingana na ukubwa wa mashamba na mapato ya mkulima kwa ujumla.
Tayari mpaka sasa mamia ya wakulima wameshafanikiwa kupata elimu ya bima ya Mazao kupitia muunganiko huo wa mashirika ya bima ambayo yamekuwa sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD) yalioanza June 26,2023 na kutamatika Julai 1,2023 mkoani Tabora.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa