Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Mhe. Mohamed Mtuliakwako, amemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, katika maadhimisho ya miaka 61 ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaliyofanyika kimkoa katika Uwanja wa Soko la National, Kata ya Kitete, Manispaa ya Tabora.
Katika hotuba yake, Mhe. Mtuliakwako alimpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa za kuwaletea wananchi maendeleo katika nyanja za kisiasa, kijamii na kiuchumi. Alibainisha kuwa mkoa wa Tabora umepokea zaidi ya shilingi bilioni 132 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya 25 za sekondari na shule 22 za msingi, pamoja na miundombinu ya vyoo, maabara, na nyumba za walimu.
Aidha, alieleza kuwa bajeti ya ununuzi wa dawa imeongezeka kutoka shilingi bilioni 4.2 mwaka 2020/2021 hadi kufikia shilingi bilioni 9.8 mwaka 2023/2024, hali ambayo imeongeza upatikanaji wa dawa katika vituo vya afya na hospitali za wilaya katika mkoa huo. Pia, ujenzi wa hospitali mpya za wilaya umeendelea kuimarika.
Mhe. Mtuliakwako alitoa rai kwa wananchi wa Tabora kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akisisitiza umuhimu wa kudumisha umoja, ushirikiano, na kuulinda Muungano ulioasisiwa na waasisi wa taifa.
“Tuna wajibu wa pamoja katika kudumisha Muungano wetu, kwani ni tunu pekee tuliyoachiwa na waasisi wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, alielezea mafanikio ya Muungano, akisisitiza kuwa mshikamano wa kiuchumi baina ya pande mbili za Muungano umeimarisha uchumi wa taifa na kuchochea maendeleo.
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Jimbo la Magharibi Tabora, Mchungaji Isaac Laizer, alitoa pongezi kwa serikali kwa hatua kubwa za maendeleo zilizopatikana, hasa katika miundombinu ya barabara, reli, uwanja wa ndege, na huduma za kijamii.
“Tanzania ambayo imelindwa kwa gharama kubwa na waasisi wetu si bahati mbaya, bali ni zawadi kutoka kwa Mungu. Tuna wajibu wa kuilinda kwa wivu mkubwa ili iendelee kuwa kisiwa cha amani,” alisema Askofu Laizer kwa msisitizo.
Maadhimisho hayo pia yaliambatana na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na usafi wa mazingira, michezo, na upandaji wa miti katika maeneo tofauti ya mkoa wa Tabora — yote yakibeba kauli mbiu:
“Muungano Wetu ni Dhamana, Heshima na Tunu ya Taifa – Shiriki Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.”
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa