Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Miundombinu, Mhandisi Faustine Mtesigwa Tarai, amefungua Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkoa wa Chief Isike Mwanakiyungi, Tabora.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa kongamano hilo, Mhandisi Tarai alisisitiza kuwa familia ni msingi wa jamii na taifa. Alibainisha kuwa changamoto zinazozikumba familia katika nyanja mbalimbali kama ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia, kiuchumi na kijinsia, zinahitaji juhudi za pamoja kupambana nazo ili kujenga taifa imara.
Mhandisi Tarai alieleza kuwa serikali inaendelea kutekeleza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na ukatili wa familia, akitaja miongoni mwa mikakati hiyo kuwa ni utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), ambapo vikundi mbalimbali vimeundwa kusaidia kutoa elimu na kuchukua hatua dhidi ya ukatili unaojitokeza.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora, Ndg. Abakos Kululetela, alieleza kuwa maadhimisho hayo yamelenga kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa familia na kuibua mijadala juu ya changamoto zinazozuia ustawi wa familia, ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia na matatizo ya kiuchumi.
Akichangia mjadala , Bi. Agneta John kutoka shirika lisilo la kiserikali la Jikomboe Integral Development Association (JIDA), alieleza kuwa taasisi yao inaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali katika kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanalelewa katika mazingira bora.
“Tunaamini kuwa namna mtoto anavyolelewa ndicho kiini cha kupata viongozi bora wa kesho. Tukibadili mwanzo wa hadithi ya maisha yao, tunaweza kubadili mustakabali mzima wa familia na taifa,” alisema Bi. Agneta.
Akihitimisha hotuba yake, Mhandisi Tarai alitoa wito kwa jamii kuhakikisha watoto wanapata malezi bora, lishe sahihi, afya njema, pamoja na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili.
“Tufanye kazi kwa bidii kupunguza umasikini katika familia zetu. Umasikini unachangia ukatili; hali duni ya maisha huwalazimisha watu kuwa wanyonge na kuvumilia ukatili usiostahili,” aliongeza.
Maadhimisho haya yalikusanya wadau mbalimbali wa maendeleo ya familia, ustawi wa jamii, pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali, huku wakiahidi kuendeleza ushirikiano katika kuboresha maisha ya familia za Kitanzania.Kauli mbiu ya maadhimisho haya kwa mwaka 2025 inasema: “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Bora”
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa