Katika kuelekea kilele cha Maadhimisho Ya Siku Ya Mbolea Duniani, Tume ya Maendeleo ya Vyama vya Ushirika Tanzania (TCDC) imeweka mikakati kuhakikisha Vyama vya Msingi (AMCOS) kutumika katika mchakato wote wa usambazaji wa mbolea ya ruzuku ili kuwafikia wakulima.
Akiongea kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TCDC, Ndugu. Venance Msafiri Mrajisi Msaidizi (M) Tabora ameeleza kuwa, idadi kubwa ya wakulima wapo vijijini ambao wamesajiliwa na wanatambulika, hivyo kupitia vyama vya Msingi wakulima watafanikiwa kupata mbolea ya ruzuku kwa urahisi.
“Asilimia kubwa ya wakulima wapo vijijini ambao wengi wao wapo kwenye vyama vya msingi, TCDC imejipanga kutumia vyama vya msingi kuhakikisha wakulima wanapata mbolea ya ruzuku kwa urahisi” alisema ndugu. Venance.
Mrajisi Msaidizi amemuhakikishia Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde, kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Wizara ya Kilimo kusimamia maslahi ya wakulima hususani kipindi hiki cha usambazaji wa mbolea ili kuhakikisha wakulima wanafaidika na mbolea hiyo.
“Napenda kukuhaikishia mheshimiwa Naibu Waziri wa Kilimo kwamba, TCDC itahakikisha inashirikiana na Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassani kupitia Wizara Ya Kilimo, kuhakikisha tunasimamia maslahi ya wakulima hususani kwenye kipindi hiki cha usambazaji wa mbolea.” Alisema Mrajisi.
Aidha, Mrajisi Venance ameeleza, ushiriki wa TCDC kwenye Maadhimisho Ya Siku Ya Mbolea Duniani, kwamba maadhimisho hayo yanagusa mkulima mmoja mmoja ambao ni sehemu ya vyama vya ushirika ambavyo navyo ni sehemu ya TCDC.
“Kwa takwimu tulizo nazo TCDC inasimamia jumla ya vyama vya ushirika elfu saba na mia tatu (7300), vyenye wanachama milioni nane (8,000,000) ambapo Vyama vya ushirika yaani AMCOS kuna wanachama 5000 ambao ni wanufaika wa maadhimisho haya ya Mbolea Duniani”
Maadhimisho ya Siku ya Mbolea Duniani, yalianza mnamo Oktoba, 11 na kuhitmishwa leo Oktoba 13, 2023 na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. David Silinde (Mb) katika viwanja vya Chipukizi, Manispaa ya Tabora, yenye kauli mbiu insemayo “Matumizi Sahihi ya Mbolea ya ruzuku kwa kilimo chenye tija”
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa