Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Lucas Magembe, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ameongoza kikao cha maandalizi ya maonesho ya wakulima – Nanenane 2025, kilichofanyika katika ukumbi wa Chief Isike Mwanakiyungi, Manispaa ya Tabora.
Kikao hicho kilihusisha viongozi pamoja na wataalamu ngazi za wilaya na mikoa kutoka mikoa ya Tabora na Kigoma,lengo ni kuweka mikakati thabiti ya kuboresha maandalizi ya maonesho ya sikukuu ya wakulima – nane nane 2025.
Akizungumza katika kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Uchumi na Uzalishaji Mkoa wa Tabora, Bw. Abraham Mndeme, aliwasilisha tathmini ya maonesho ya mwaka 2024 na kubainisha kuwa Manispaa ya Kigoma iliibuka mshindi wa kwanza kati ya washiriki wote wa kanda ya magharibi.
Katika kikao hicho, wajumbe waliagizwa kuwajulisha Wakurugenzi Watendaji wa halmashauri zote za Tabora na Kigoma kuanza mapema maandalizi ya maonesho hayo, ikiwa ni pamoja na kuandaa mpango kazi mahsusi wa maonesho ili kuwavutia wawekezaji zaidi. Wadau pia walihimizwa kuwaelimisha wakulima, wafugaji na wavuvi kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa ili kuongeza tija na ubora katika uzalishaji
.
Akihitimisha kikao hicho, Mhe. Magembe alibainisha maazimio kadhaa yaliyopitishwa na wajumbe, likiwemo pendekezo la wadau wa maonesho kuchangia vitu halisi badala ya fedha, ili kurahisisha utekelezaji wa shughuli kwa wakati.
“Tumegundua kuwa michango ya kifedha huchukua muda mrefu kufanikishwa kutokana na taratibu za kifedha. Kwa kuchangia vifaa na huduma moja kwa moja, tutaokoa muda na kuongeza ufanisi,” alisema Mhe. Magembe.
Aidha, upatikanaji wa huduma ya maji ya uhakika katika eneo la maonesho umetajwa kuwa kipaumbele ili kuwezesha maandalizi ya vitalu vya maonesho kwa ufanisi.
Mhe. Magembe aliwashukuru wajumbe kwa michango yao, akisema kuwa maazimio ya kikao hicho yatasaidia kuboresha kwa kiwango kikubwa maonesho ya mwaka huu.
Maonesho ya Nanenane kwa kanda ya Magharibi yanatarajiwa kufanyika katika viwanja vya Ipuli, Manispaa ya Tabora, yakijumuisha mikoa ya Tabora na Kigoma, huku maadhimisho ya kitaifa yakifanyika jijini Dodoma.
Kaulimbiu ya mwaka huu ni: "Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025."
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa