Na. OMM - Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Mhe. Cornel Lucas Magembe, amewataka wajasiriamali wa Mkoa wa Tabora kutumia maarifa waliyojifunza kuboresha uzalishaji wa bidhaa zao na kukuza uchumi wao pamoja na wa Taifa.
Akizungumza katika hafla ya kufunga mafunzo maalum ya ujasiriamali yaliyofanyika katika Nyumba ya Ujasiriamali Kitete, Mhe. Magembe alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, na kusisitiza umuhimu wa kuyatumia mafunzo hayo kuboresha bidhaa ili ziweze kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mafunzo hayo ya siku saba yaliandaliwa na kikundi cha ujasiriamali cha Grows Global Innovations Company Limited kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO) Mkoa wa Tabora. Bi. Ashura Shabani Mwazembe, Mwenyekiti wa Grows Global Innovations, alisema kuwa lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwajengea uwezo wajasiriamali pamoja na wananchi wanaotamani kuingia katika sekta hiyo kwa kuwapatia maarifa juu ya utengenezaji wa sabuni za maji,sabuni za miche,marashi mbalimbali, usindikaji wa matunda na mbogamboga, ufugaji wa nyuki na usindikaji wa mazao ya nyuki, pamoja na mbinu za kuongeza thamani ya bidhaa katika soko.
Mafunzo hayo yaliendeshwa na mtaalamu mahiri wa ujasiriamali nchini, Dkt. Ladislaus Luambano (Baba wa Wajasiriamali) kutoka Dar es Salaam.
Kwa upande wake, Meneja wa SIDO Mkoa wa Tabora, Bw. Samwel Neligwa, alikipongeza kikundi cha Grows Global Innovations kwa juhudi zao za kuandaa mafunzo haya, akisema kuwa yatawasaidia wajasiriamali kuinuka kiuwezo na kiuchumi, hivyo kuwawezesha kushindana katika masoko mbalimbali.
Akifunga rasmi mafunzo hayo, Mhe. Magembe alimpongeza Bi. Ashura Mwazembe kwa juhudi zake za kutafuta maarifa na ujuzi zaidi kwa ajili ya kuendeleza wajasiriamali wa Tabora. Aliwasihi wahitimu kutumia ujuzi waliopata si tu kwa manufaa yao binafsi, bali pia kwa maendeleo ya mkoa na taifa kwa ujumla.
Mafunzo haya yalifunguliwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, na kufungwa na Mhe. Magembe kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa. Hafla hiyo ilihitimishwa kwa utoaji wa vyeti kwa wahitimu zaidi ya ishirini waliofanikiwa kuhitimu mafunzo hayo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa