Maelfu ya wakristo wa Jimbo Kuu Katoliki la Tabora wameungana katika ibada takatifu ya Alhamisi Kuu iliyoongozwa na Baba Askofu Mkuu, Muadhama Kardinali Protase Rugambwa, katika Kanisa la Mtakatifu Theresia Mtoto Yesu.
Katika mahubiri yake, Kardinali Rugambwa ametoa wito kwa waumini na Watanzania kwa ujumla kuishi kwa mujibu wa mafundisho ya Yesu Kristo, hususan kwa kuonesha upendo wa kweli, kujitolea kwa ajili ya wengine, na kutunza amani ya taifa.
“Tujitoe ndugu zangu, kila mmoja kwa kile alichonacho – kwa hali na mali. Tusifanye tu yale yanayotunufaisha sisi na watu wa karibu yetu pekee, bali tumsaidie hata yule ambaye hatumfahamu au ambaye ni tofauti nasi, kama Kristo alivyowaosha miguu hata wale waliomsaliti,” alisisitiza Kardinali Rugambwa.
Ameongeza kuwa kujitolea kwa dhati na kuwapenda watu wote – wema kwa waovu – ndicho kiini cha ujumbe wa Kristo, ambaye hakubagua hata wale waliokuwa na nia ya kumsaliti.
Mbali na mafundisho ya kiroho, Kardinali Rugambwa amegusia hali ya kijamii na kisiasa, akisisitiza umuhimu wa kutunza amani ya taifa kwa njia ya maridhiano, kusikilizana, na kuondoa matusi au malumbano yenye kuleta mgawanyiko.
“Hata katika siasa, tunapaswa kutumia Imani yetu kuleta maridhiano, siyo kuchochea chuki. Tukumbatie tofauti zetu kwa njia ya mazungumzo, siyo mivutano. Hapo ndipo tunapotimiza upendo wa Kristo,” alieleza.
Ibada hiyo ya Alhamisi Kuu ilihidhuliwa na Mkuu wa mkoa wa Tabora Mheshimwa Paul Chacha ilihusisha pia zoezi la kuosha miguu kwa wafuasi wa Yesu, likiwa ni ishara ya unyenyekevu na huduma. Miongoni mwa waliooshwa miguu ni Katibu Tawala wa Mkoa huo, Dkt. John Mboya.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa