Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto Duniani (UNICEF) imezindua mafunzo maalum kwa Maafisa Elimu Sekondari, Maafisa Maendeleo ya Jamii, Waratibu wa UNICEF, na walimu mahili wa masomo ya Sayansi. Mafunzo haya yanafanyika katika ukumbi wa maktaba wa Shule ya Wavulana Tabora, yanalenga kuboresha mbinu za ufundishaji na kuongeza hamasa kwa wanafunzi, hasa wa kike, kusoma masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM).
Akifungua rasmi mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa, Katibu Tawala Msaidizi Miundombinu, Mhandisi Faustine Tarai, alisema kuwa mwitikio wa wanafunzi katika kusoma masomo ya Sayansi bado ni mdogo, hasa kwa somo la Hisabati. Alieleza kuwa tatizo hili linaanzia shule za msingi, ambapo watoto wengi hujenga hofu dhidi ya masomo haya kutokana na ukosefu wa mazingira rafiki ya kujifunza na kutokuwepo kwa hamasa ya kutosha.
Takwimu za mwaka 2024 zinaonyesha kuwa kati ya wanafunzi 15,125 waliomaliza Kidato cha Nne, ni asilimia 24 pekee waliosoma masomo ya Sayansi, ikiwa ni sawa na wanafunzi 3,596. Kati yao, wasichana walikuwa 1,596, hali inayoashiria uwiano mdogo wa wanafunzi wa kike katika masomo ya Sayansi. Hali hii ni sawa pia katika masomo ya Hisabati na Kemia, ambapo idadi ya wanafunzi wa kike bado ni ndogo ukilinganisha na ya wavulana.
Serikali na UNICEF zinahimiza wadau wa elimu kuweka mikakati madhubuti ili kuongeza hamasa kwa wanafunzi, hususan wa kike, kujikita katika masomo ya Sayansi. Mhandisi Tarai alieleza kuwa baadhi ya mbinu zinazopendekezwa ni: Kuboresha upatikanaji wa vifaa vya maabara katika shule za sekondari, Kutoa hamasa kwa walimu na wanafunzi ili kuvunja dhana potofu ya kuwa masomo ya Sayansi ni magumu, Kuhakikisha matumizi sahihi ya rasilimali zilizotolewa kwa ajili ya elimu ya Sayansi, Kuimarisha upangaji wa bajeti kwa ajili ya maendeleo ya elimu ya Sayansi, ikiwemo matumizi ya fedha kutoka serikali kuu pamoja na na mapato ya ndani ya halmashauri.
Kwa upande wao, walimu walioshiriki mafunzo hayo wameipongeza serikali na UNICEF kwa juhudi zao katika kuboresha elimu ya Sayansi nchini, wakiahidi kutumia ujuzi watakaopata kuhamasisha wanafunzi zaidi, hasa wa kike, kupenda masomo ya sayansi.
Akihitimisha hotuba yake, Mhandisi Tarai alisisitiza kuwa dunia ya sasa na inayokuja inahitaji wataalamu wa Sayansi na Teknolojia. Aliitaka jamii nzima kushiriki katika juhudi za kuwahamasisha wanafunzi wa kike kujikita katika masomo ya sayansi ili kuongeza idadi ya wasichana wanaochagua masomo hayo na kupata watalaam wengi wa taaluma za sayansi kwa wakati ujao.
Mafunzo haya, yanayotarajiwa kudumu kwa siku tatu, yanapewa matumaini makubwa ya kuleta mabadiliko chanya katika elimu ya Sayansi nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa