Mkuu wa Wilaya ya Nzega, Mhe. Naitapwaki Lemei Tukai, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amewapokea rasmi wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Misitu Tanzania waliowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi. Ujumbe huo umeongozwa na Mwenyekiti wa Bodi, Prof. Shabani Chamshama, ambapo lengo la ziara hiyo ni kukagua na kujionea maendeleo ya miradi inayofadhiliwa na mfuko huo katika mkoa wa Tabora.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa moja ya miradi hiyo – ujenzi wa kiwanda kidogo cha kuchakata mazao ya nyuki katika kijiji cha Nkiniziwa, wilayani Nzega – Kamanda wa Kanda Msaidizi Maendeleo ya Ufugaji Nyuki, Ndg. Nuru Tengeza, amesema mradi huo unalenga kuongeza thamani ya mazao ya nyuki kwa kuwawezesha wafugaji kupata bidhaa bora zilizochakatwa.
“Kiwanda hiki pia kitakuwa kituo cha kutoa mafunzo kwa jamii na wadau wa sekta ya nyuki, kikishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania. Tumeandaa mpango wa kuanzisha shamba darasa katika eneo la msitu jirani,” alisema Tengeza.
Kiwanda hicho kimejengwa kwa ufadhili wa shilingi milioni 111.3 kutoka Mfuko wa Misitu Tanzania na tayari ujenzi wake umekamilika.
Wajumbe wa bodi pia walitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la mihadhara katika Chuo cha Mafunzo ya Ufugaji Nyuki Tabora, mradi unaogharimu shilingi milioni 592.1 – ambapo shilingi milioni 500 zimetolewa na Mfuko wa Misitu Tanzania. Hadi sasa, ujenzi huo umefikia asilimia 55.
Mkuu wa Chuo hicho, Ndg. Seme Daudi, amesema kukamilika kwa jengo hilo kutaboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza udahili wa wanafunzi watakaoendeleza sekta ya nyuki kitaalamu.
Ziara hiyo ilihitimishwa kwa kutembelea eneo la mradi wa ujenzi wa Kituo cha Utafiti wa Misitu (TAFORI) Kanda ya Magharibi, katika kijiji cha Kipalapala,nje kidogo ya mji wa Tabora. Bodi imeeleza kuridhishwa na hatua za awali za maandalizi ya eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 10.
Kaimu Meneja wa kituo hicho, James Lyamuya, pamoja na viongozi wengine wa miradi, wamepokea maelekezo ya msingi kutoka kwa bodi na kuahidi kuyatekeleza kikamilifu kwa kuzingatia sheria za ununuzi wa umma na kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora na kwa wakati.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa