Na. Mwandishi Wetu, Tabora.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Mhe. Dkt. Gelard Mongella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ameongoza kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe, usafi wa mazingira pamoja na malezi na makuzi ngazi ya mkoa, kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Akifungua kikao hicho, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Ndg. John Mboya, aliwapongeza wadau wa sekta ya afya, elimu na maendeleo ya jamii kwa ushirikiano wao uliowezesha mkoa kupata alama ya kijani katika utekelezaji wa afua za lishe.
“Kwa hiyo niwapongeze sana kwa kazi nzuri mlioifanya… sasa tunaona green! Hii green ni jambo la kujivunia, hongereni sana,” alisema Dkt.Mboya.
Akizungumza na washiriki wa kikao hicho, Mhe. Dkt. Mongella aliwapongeza wataalamu na viongozi wa halmashauri kwa kazi kubwa waliyoifanya, huku akisisitiza haja ya kuongeza nguvu ili mkoa uendelee kubaki katika daraja la kijani.
“Kwa bidii tuliyoifanya na malengo tuliyowekeana, tuhakikishe tunapanda juu zaidi. Tutumie takwimu tulizonazo kuziba mapungufu yaliyopo ili Tabora iwe kinara katika masuala ya lishe, uchumi na ustawi wa wananchi wake,” alisisitiza Mhe. Mongella
Katika mjadala wa kikao hicho, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Afya mkoani Tabora, Dkt. Honoratha Rutatanisibwa, alieleza kuwa changamoto ya kupasuka kizazi kwa akina mama wajawazito inachangiwa na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, matumizi ya dawa za asili kwa ajili ya kuongeza uchungu, ushiriki mdogo wa wenza katika kipindi cha ujauzito hadi kujifungua, na kushindwa kuhudhuria kliniki mapema ili kubaini viashiria vya hatari vya uzazi pingamizi.
Dkt. Rutatanisibwa alitoa rai kwa jamii, hususan wanaume, kuwa karibu na wake zao kipindi chote cha ujauzito hadi kujifungua, akisema hatua hiyo itasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wakurugenzi wa Halmashauri mkoani Tabora, Dkt. John Pima, alihimiza wadau na jamii kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu afya ya uzazi ili kuokoa maisha.
Kikao hicho kilihitimishwa kwa utoaji wa vyeti vya pongezi kwa shule na hospitali zilizofanya vizuri katika kuhamasisha lishe bora kupitia bustani za mbogamboga na matunda. Halmashauri za Uyui, Kaliua na Igunga zilitajwa kuwa mfano bora kwa utekelezaji huo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa