Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), kwa kushirikiana na wadau wa mazingira nchini, wameandaa mafunzo maalum kuhusu Mbinu Jumuishi ya Tathmini ya Mazingira na Udhibiti wa Uharibifu wa Ardhi pamoja na kupotea kwa bioanuwai katika misitu ya miombo iliyo kusini magharibi mwa Tanzania. Mafunzo hayo yamefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya JB, mjini Tabora.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, mgeni rasmi Dkt. Deogratias Paul Nyangu alisema kuwa mafunzo hayo ni ya muhimu kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa mkataba wa kimataifa wa kupambana na hali ya jangwa. Alisisitiza kuwa ni wajibu wa wadau wa mazingira kujifunza na kuwa tayari kuchukua hatua madhubuti kushiriki kikamilifu katika vita dhidi ya uharibifu wa ardhi katika maeneo yao.
Mafunzo haya ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Misitu ya Miombo katika mikoa ya Tabora na Katavi. Mradi huu ulianza Januari 2023 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2027. Jumla ya washiriki 60 wamehudhuria mafunzo hayo, wakitoka katika halmashauri nne: Mlele, Sikonge, Urambo na Kaliua.
Washiriki wa warsha hiyo ni pamoja na maafisa waandamizi kutoka TFS, wahadhiri wa vyuo vikuu na wawakilishi kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais. Lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo washiriki kutambua hali halisi ya maeneo yaliyoathirika na uharibifu wa ardhi na misitu, pamoja na kuandaa mikakati madhubuti ya kupunguza au kuondoa kabisa changamoto hiyo.
Mafunzo hayo pia yanatumia mbinu za kisasa katika uchambuzi wa taarifa, zikiwemo teknolojia ya mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS), ili kubaini maeneo hatarishi na kupanga mipango ya kurekebisha hali ya mazingira.
Mradi huu muhimu unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF) pamoja na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa