KAMPENI YA KISOMO CHA ELIMU YA WATU WAZIMA YAANZA KWA NGUVU MPYA TABORA.
Katika hali ya kuamsha ari ya elimu kwa watu wazima nchini, Kampeni ya Uanzishaji na Uimarishaji wa Madarasa ya Kisomo imezinduliwa rasmi mkoani Tabora, ikiwa ni hatua mahsusi ya kitaifa inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya pili ya kujifunza. Uzinduzi huu umeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Mhe. Khamis Mkanachi, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, ambapo pamoja na viongozi wengine na wananchi, walijumuika kuonesha mshikamano wa kweli katika kutokomeza ujinga na kuongeza ujuzi miongoni mwa watu wazima.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mkanachi alisisitiza kuwa elimu ya watu wazima si hiari tena bali ni hitaji la msingi kwa maendeleo ya taifa. Alieleza kuwa takwimu za asilimia 32 ya watu wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu mkoani Tabora ni changamoto kubwa inayohitaji hatua za dharura. Alieleza kuwa Serikali kupitia Dira ya Maendeleo ya 2050 na mwelekeo wa Ajenda ya Afrika 2063, imeweka mkazo mkubwa katika kujenga jamii yenye maarifa, ujuzi na usawa wa kijinsia, na kwamba elimu jumuishi kwa watu wote ni nyenzo muhimu ya kufanikisha ajenda hizo.
Naye Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima nchini (TEWW), Prof. Philipo Sanga, aliweka bayana kuwa taasisi yake imekuwa kinara katika utekelezaji wa mikakati ya kitaifa kupitia programu kama MUKEJA na mbinu ya RIFLEKTI inayowalenga watu wazima katika kupata stadi si tu za KKK, bali pia ujuzi wa maisha, ujasiriamali na utatuzi wa changamoto za kijamii. Alisema kuwa TEWW imeendelea kutoa mafunzo kwa wakufunzi na wawezeshaji kote nchini ili kuongeza ufanisi wa programu hizi, huku lengo kuu likiwa ni kuhakikisha hakuna Mtanzania anayebaki nyuma kielimu.
Aidha, Mhe. Mkanachi alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuwekeza kwa kiwango kikubwa katika elimu, ikiwemo elimu nje ya mfumo rasmi. Alitaja Waraka wa Elimu Na. 2 wa mwaka 2021 kuwa mfano wa jitihada hizo, ambapo mabinti waliokatisha masomo wanapewa fursa ya kurejea na kujiendeleza. Alitoa rai kwa halmashauri, taasisi, mashirika binafsi na wadau wa maendeleo kushiriki kwa hali na mali katika kuanzisha na kuimarisha madarasa ya kisomo.
Kwa upande wake, Prof. Sanga alisisitiza kuwa pamoja na mafanikio yaliyopo, bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi hususani katika maeneo ya vijijini na pembezoni mwa jamii ambako uhitaji wa elimu ni mkubwa. Aliongeza kuwa kampeni hii ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 50 ya TEWW, na inalenga kuwasha tena taa ya matumaini kwa maelfu ya Watanzania waliokata tamaa ya kujifunza. Kauli mbiu ya “Elimu Haina Mwisho” imepewa uhai upya kupitia kampeni hii.
Mwisho, kwa niaba ya Mkoa wa Tabora, Mhe. Mkanachi aliahidi kuwa serikali ya mkoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na TEWW katika kuhakikisha ajenda hii muhimu ya elimu ya watu wazima inatekelezwa kikamilifu. Alisisitiza kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana bila elimu, na hivyo kila mmoja anapaswa kuwa balozi wa kusambaza hamasa ya kisomo katika jamii. Katika kutamatisha hafla hiyo, alitangaza rasmi kuzinduliwa kwa kampeni ya kuanzisha na kuimarisha madarasa ya kisomo nchini kote.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa