Mkuu wa mkoa wa Kigoma IGP (Mstaafu) Balozi Simon Nyakoro Sirro, amehitimisha rasmi maonesho ya sikukuu ya wakulima nane nane yaliyofanyika kikanda mkoani Tabora katika viwanja vya Fatma Mwasa,Ipuli – Manispaa ya Tabora. . Katika hotuba yake, Balozi Sirro alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi, pamoja na wadau wote walioshiriki kufanikisha maonesho haya.
Akizungumzia kaulimbiu ya mwaka huu “Chagua Viongozi Bora kwa Maendeleo Endelevu ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi 2025”, Balozi Sirro aliwahimiza wananchi wa Tabora na Kigoma kujitokeza kwa wingi katika uchaguzi ujao, wakichagua viongozi watakaosimamia maendeleo ya sekta hizo. Alisisitiza umuhimu wa kutumia elimu, teknolojia na ubunifu uliopatikana kupitia maonesho haya ili kuongeza tija na thamani katika uzalishaji.
Kwa upande wa kilimo, alieleza hatua za Serikali katika kutoa mbolea na mbegu bora kwa ruzuku, kuhakikisha upatikanaji wa pembejeo kwa wakati, na kuimarisha taasisi za utafiti kama TARI na SUA. Aidha, aliwasihi wakulima kujiandikisha ili kuendelea kunufaika na mpango wa ruzuku na kutumia mbegu zenye ubora unaodhibitiwa na mamlaka husika.
Katika sekta ya mifugo, alibainisha kampeni kubwa ya chanjo iliyoanzishwa na Rais Samia, ikilenga kupunguza vifo na magonjwa ya mifugo. Wafugaji walihimizwa kuchangamkia huduma za taasisi za serikali ikiwemo TVLA na ZVC, ili kupata huduma za chanjo, uchunguzi wa magonjwa, vibali na mafunzo ya ufugaji bora. Sekta ya uvuvi na ufugaji nyuki pia zilitajwa kama maeneo yenye fursa kubwa, zikichochewa na uwepo wa vituo maalum vya mafunzo na uzalishaji katika kanda.
Balozi Sirro pia amesisitiza kuboresha namna wakulima wanavyofungasha bidhaa zao kwa kutumia vifungashio bora lakini vilivyobeba thamani ya bidhaa yenyewe, ikiwemo kuonesha aina ya virutubisho au madini yaliyomo. Amewashauri wakulima kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ili kuhakikisha bidhaa wanazozalisha zinakidhi viwango na ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa, hatua itakayoongeza ushindani kwenye masoko ya ndani na nje ya nchi.
Akihitimisha, alisisitiza umuhimu wa kuongeza thamani ya mazao, kuimarisha mabanda ya kudumu, na kuandaa mikakati ya matumizi endelevu ya viwanja vya maonesho mwaka mzima. Aliwataka makampuni ya mawasiliano na taasisi za kifedha kushirikiana katika kudhamini maonesho haya ili kuongeza ushiriki na kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji na wavuvi. “Maadhimisho haya ya Nanenane Kanda ya Magharibi kwa mwaka 2025 yamefikia kilele chake leo,” alitangaza huku akipokea shangwe za washiriki na wananchi.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa