Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Upendo Bert Wella, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Paulo Chacha, leo amemkabidhi bondia wa uzito wa kati, Abdul Zugo (Abdul Kessy Kasongo), fedha taslimu shilingi milioni 10. Fedha hizo ni sehemu ya ahadi ya shilingi milioni 15 aliyoitoa RC Chacha, ambapo tayari awali alimpatia shilingi milioni 5 kumwezesha maandalizi ya pambano kubwa la kuwania mkanda wa Ubingwa wa Mabara.
Zugo anatarajiwa kupanda ulingoni kesho, Agosti 23, 2025, dhidi ya bondia kutoka India, Sameer Kumar, katika pambano litakalofanyika majira ya jioni kwenye ukumbi wa Tabora Hotel, mjini Tabora.
Sambamba na tukio hilo la kukabidhi fedha, mabondia wote walipima afya na uzito kulingana na kanuni za Shirikisho la Ngumi Duniani (WBC), hatua muhimu kabla ya mashindano ya kimataifa.
Pambano hilo kubwa litapambwa na mapambano ya utangulizi yakihusisha mabondia kadhaa kutoka ndani na nje ya mkoa wa Tabora. Mojawapo ya mapambano yaliyovuta hisia ni kati ya Karim “Mtu Kazi” Mandonga na Juma Farahani, ambao leo walitambiana vikali wakati wa upimaji wa afya na uzito, hali iliyoongeza hamasa na mvuto wa mashindano hayo.
Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Wella, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushuhudia pambano hilo la kihistoria, huku akisisitiza umuhimu wa kuwaunga mkono vijana wa Kitanzania wanaopeperusha bendera ya taifa kupitia michezo ya ngumi.
“Huu ni wakati wa kuonyesha mshikamano wetu kama Watanzania. Vijana wetu kama Abdul Zugo na Juma Farahani wanapigania heshima ya mkoa wa Tabora na taifa kwa ujumla, hivyo tushiriki kuwatia moyo,” alisema.
Wakazi wa Tabora na vitongoji vyake wanatarajiwa kufurika ukumbini kushuhudia burudani hii kabambe, ambapo ushindi wa mabondia wa ndani unaweza kufungua milango mipya ya kimataifa kwa mchezo wa ngumi nchini Tanzania.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa