Kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Honoratha Rutatinisibwa, amefungua kikao cha tathmini ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT–MMMAM) kwa kipindi cha Januari hadi Juni 2025. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Dkt. Rutatinisibwa alisisitiza wajibu wa jamii katika kuhakikisha usalama na ustawi wa mtoto, akibainisha kuwa taifa lenye maendeleo linajengwa kwa msingi wa malezi bora na ulinzi wa watoto. Alionya dhidi ya kufumbia macho vitendo vya ukatili ikiwemo ubakaji, ulawiti na adhabu zisizofaa, akisisitiza kuwa sheria na sera zinazolinda haki za watoto zinapaswa kuheshimiwa.
“Tunapaswa kuhakikisha kila mtoto analelewa katika mazingira salama, yenye maadili na yanayomwezesha kufanikisha ndoto zake. Serikali itaendelea kusimamia haki za watoto kwa dhati, ili taifa letu lijenge kizazi chenye kuleta tija kwa maendeleo,” alisema Dkt. Rutatinisibwa.
Mratibu wa programu ya Mtoto Kwanza kutoka shirika lisilokuwa la kiserikali la JIDA, Bi. Agneta John, alisema mpango huo unalenga kuhakikisha watoto wanapata huduma bora katika maeneo ya afya, lishe, malezi yenye mwitikio, fursa za ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi na usalama wa mtoto. Alieleza kuwa utekelezaji wake mkoani Tabora umefanikiwa kutokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali.
Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Tabora, Bw. Abakos Deodatus, alieleza kuwa juhudi za pamoja zimewezesha kufikiwa kwa shule za msingi na sekondari 191, ambapo elimu ya ulinzi na usalama wa mtoto imetolewa kwa wanafunzi 35,314, walimu wakuu 264 na maafisa elimu kata 206. Aidha, kampeni za kupinga ukatili zimeenezwa kupitia vyombo vya habari, huku watoto 151 waliokuwa mitaani wakibainika, ambapo 134 wamerejeshwa kwa wazazi wao na 17 wamepata hifadhi kwenye vituo vya kulea watoto yatima.
Katika kikao hicho, wadau wa malezi ya mtoto walikubaliana kuongeza kasi na umakini katika kumlinda mtoto dhidi ya changamoto zinazomkabili nyumbani, shuleni na mitaani, kwa lengo la kujenga kizazi chenye afya, usalama na mchango chanya kwa maendeleo ya taifa.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa