Katika juhudi za kuimarisha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paulo Matiko Chacha, amekabidhi rasmi magari sita aina ya Toyota Land Cruiser kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi (SACP) Richard Abwao.
Hafla hiyo imefanyika katika uwanja wa nje ya Ofisi ya Ukumbi wa Mikutano wa Chief Isike Mwanakiyungi, Tabora, ambapo magari hayo yametolewa kwa ajili ya kusaidia kazi za doria, misako na oparesheni mbalimbali za kiusalama katika mkoa huo.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, RC Chacha amesema:
“Magari haya ni kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa Jeshi letu la Polisi. Mheshimiwa Rais ataendelea kuleta magari zaidi kwa ajili ya idara ya upelelezi na vikosi vya FFU katika wilaya zote. Ni wajibu wetu kuyatunza magari haya na kuhakikisha yanatumika kwa kazi maalum zilizokusudiwa. Tuendelee kuwalinda wananchi wa Tabora, ambao tumekabidhiwa jukumu la kuhakikisha usalama wao wakati wote.”
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, ameishukuru serikali kwa msaada huo akisema:
“Kupokea magari haya sita kutoka kwa Mkuu wa Mkoa ni faraja kubwa kwetu. Magari haya yatagawanywa kwa wakuu wa polisi wa wilaya zote, jambo litakalopunguza kwa kiasi kikubwa changamoto tulizokuwa nazo. Namshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutupatia magari haya, pamoja na IGP kwa kutugawia, na Mheshimiwa Chacha kwa kuyakabidhi rasmi hapa Tabora. Tumejipanga kuhakikisha magari haya yanatunzwa na kutumika ipasavyo kwa malengo yaliyokusudiwa.”
Magari haya yanatarajiwa kuongeza ufanisi katika shughuli za kiusalama mkoani Tabora, ikiwa ni pamoja na kuwezesha doria za mara kwa mara, oparesheni za kiintelijensia na kuimarisha uwezo wa kuwahudumia wananchi kwa haraka zaidi.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa