Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Mashaka Biteko ameongoza hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa kiwanda kipya cha kuzalisha nguzo za zege cha TCPM (Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company Limited), kilichopo mkoani Tabora – hatua kubwa katika safari ya Tanzania kuelekea kuwa na uhakika wa nishati ya umeme.
Akizungumza katika hafla hiyo, Meneja Mkuu wa TCPM, Ndg. Yusuph Kitivo alieleza kuwa ujenzi wa kiwanda hicho ulianza rasmi tarehe 30 Oktoba 2024, mara baada ya kusainiwa kwa mkataba baina ya kampuni hiyo tanzu ya TANESCO na wakandarasi wazawa — Msangi Enterprises na Bahari Construction Company Ltd.
Mradi huo unaogharimu shilingi bilioni 6.8 umefikia asilimia 75 ya utekelezaji, na unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 30 Juni 2025. Kufuatia ukamilikaji wake, kiwanda hicho kitaanza uzalishaji rasmi mwezi Julai mwaka huu, kikitarajiwa kuzalisha wastani wa nguzo 120 kwa siku. Hii ni sehemu ya juhudi za serikali ya awamu ya sita kuhakikisha nchi inakuwa na mfumo madhubuti wa usambazaji wa nishati kwa kutumia vifaa vya kudumu na vya kisasa.
Akitoa salamu za chama, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Nkumba, aliipongeza wizara ya Nishati kwa jitihada inazozifanya katika kusambaza umeme vijijini na mijini. Alisisitiza kuwa CCM itaendelea kuwa mstari wa mbele kuwaletea wananchi maendeleo na kuwapatia wagombea wanaokubalika na jamii.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa unaoendelea mkoani humo, akisema mradi huo utazalisha ajira na kuchochea uchumi wa wananchi wa Tabora.
Wabunge wa mkoa huo pia walitoa shukrani zao kwa serikali, huku Mhe. Munde Tambwe (Mbunge wa Viti Maalum) akiomba serikali kuanzisha kiwanda cha kuchakata tumbaku na kufufua kiwanda cha nyuzi, akibainisha kuwa Tabora ina uzalishaji mkubwa wa tumbaku na pamba. Naye Mhe. Emmanuel Mwakasaka (Mbunge wa Tabora Mjini) aliitaka serikali kutazama upya gharama za kuunganisha umeme kwa wakazi wa vijijini, hususan maeneo ya pembezoni mwa mji wa Tabora.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Mhe. Dkt. Biteko aliipongeza serikali ya awamu ya sita kwa jitihada kubwa za kuimarisha sekta ya nishati. Alisisitiza kuwa Dkt. Samia Suluhu Hassan anatamani kuona matokeo halisi, si maneno matupu, katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Ametoa rai kwa wananchi kuanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa ajili ya kulinda afya zao na kuhifadhi mazingira. Aidha, alikumbusha umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi kwa kujitokeza kujiandikisha, kuhudhuria kampeni kwa amani, na hatimaye kupiga kura kwa kuzingatia sera na kazi za wagombea badala ya matusi na mipasuko ya kisiasa.
Hafla hii imehitimisha ziara ya siku mbili ya Naibu Waziri Mkuu mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya msisitizo wa serikali katika kuimarisha miundombinu ya nishati nchini kwa maendeleo endelevu.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa