Katika jitihada za kuimarisha afya ya mama na mtoto, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora imeendesha kikao kazi maalum cha kupokea mrejesho wa mafunzo elekezi kwa watoa huduma za afya ya uzazi na mtoto, pamoja na taarifa ya mapitio ya vifo vya uzazi na vya watoto wachanga vilivyofanyika katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chief Isike Mwanakiyungi mjini Tabora, kikihusisha wadau muhimu katika ngazi ya mkoa na wilaya, wakiwemo timu ya usimamizi wa huduma za afya mkoa, Waganga Wakuu wa Wilaya, Wauguzi Wakuu, Waratibu wa Huduma za Mama na Mtoto, Makatibu wa Afya wa Wilaya, pamoja na Waganga na Wauguzi Wafawidhi kutoka hospitali na vituo vya afya wa hospitali za serikali na zile za watu binafsi.
Kupitia kikao hicho, Serikali ya Mkoa wa Tabora imeonesha dhamira thabiti ya kuboresha huduma za afya ya uzazi na mtoto, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha huduma bora, zenye staha na zenye kuzingatia muktadha wa kijamii zinapatikana kwa wanawake wajawazito na watoto wachanga.
Takwimu zilizowasilishwa na Wizara ya Afya zinaonesha mafanikio makubwa kitaifa, ambapo kiwango cha vifo vya wanawake wajawazito kimepungua kwa asilimia 80 — kutoka vifo 556 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2016 hadi vifo 104 mwaka 2022. Hii ni hatua ya kihistoria kuelekea kufikia lengo la Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (SDG) la kupunguza vifo hadi visivyozidi 70 kwa kila vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030.
Kwa kuendesha mapitio ya kina na kupanga hatua za kimkakati, Mkoa wa Tabora umejiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na vifo vya mama na mtoto — tatizo ambalo linapoteza maisha ya maelfu ya wanawake na watoto kila mwaka barani Afrika. Ufuatiliaji endelevu, ushirikiano na dhamira ya kisiasa vitakuwa nguzo kuu za mabadiliko ya kweli katika sekta ya afya.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa