Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, ametembelea Shule ya Wasichana Tabora kwa lengo la kuzungumza na uongozi wa shule hiyo pamoja na wazazi, kufuatia mfululizo wa matukio yaliyoibua sintofahamu kuhusu mwenendo wa nidhamu na uongozi katika shule hiyo ya kihistoria.
.
Akitoa taarifa rasmi ya uchunguzi, Katibu Tawala wa Mkoa, Dkt. John Mboya, alieleza kuwa mwanafunzi wa shule hiyo ambaye jina lake na taarifa zake zimehifadhiwa kwa mujibu wa sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, mwanafunzi huyo alitoa taarifa ya kuumwa na akapelekwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa Kitete,lakini baada ya kupokelewa, kabla majibu ya vipimo vyake kutoka alibainika kuwa alijifungua katika maliwato ya hospitalini hapo hali ambayo iliulazimu uongozi wa wilaya na mkoa ukiongozwa na Katibu Tawala mkoa kuunda timu maalum kufanya uchunguzi juu ya hali hiyo na mwenendo mzima wa uendeshaji wa shule hiyo.
Taarifa ya uchunguzi ilibaini kuwa mwanafunzi huyo aliripoti shuleni hapo akiwa na ujauzito—lakini cha kushtua zaidi ni kuwa hakuna mwalimu wala kiongozi yeyote wa shule aliyeweza kugundua hali hiyo hadi kufikia hatua ya kujifungua.
“Tabia ya baadhi ya wanafunzi kujihusisha na ngono wakiwa bado shuleni ni jambo linaloumiza sana. Wazazi tunapaswa kushirikiana kwa nguvu katika malezi ya watoto wetu wa kike.”Alieleza Dkt. Mboya
Uchunguzi huo pia ulibaini kuwa hali ya utendaji shuleni hapo imeathiriwa na hali ya baadhi ya walimu kukaa kwa muda mrefu katika kituo kimoja cha kazi bila uhamisho hali ambayo imesababisha mazoea, kuvuja kwa maadili ya kazi, na kudhoofisha uongozi.
Akizungumza mbele ya walimu na wazazi wa shule hiyo, Mhe. Paul Chacha hakuficha masikitiko yake kuhusu hali ya shule hiyo:
“Kama mtu ana miaka 17 hapa,hii ina maana ni umri wa tangu mtoto anazaliwa mpaka anafika kidato cha sita, alishazoea hata darasani haendi, hana haja ya kujua nidhamu ya mtoto ikoje, mwalimu wa darasa haingii na hana haja ya kujua darasa hilo linaendeleaje? Tatizo lililopo ni watu kufanya kazi kwa mazoea,” Mhe. Chacha alisema kwa masikitiko.
Mhe. Chacha alitoa maagizo ya kuwa walimu wote waliodumu shuleni hapo kwa muda mrefu bila kuhamishwa wachukuliwe hatua za kupelekwa vituo vingine vya kazi. Mhudumu wa afya aliyehusika na ujazaji wa fomu ya uchunguzi wa afya ya mwanafunzi huyo achukuliwe hatua za kisheria kwa uzembe aliouonesha. Ufuatiliaji wa karibu ufanyike ili kubaini aliyesababisha ujauzito wa mwanafunzi huyo na sheria ichukue mkondo wake.
Vilevile Binti huyo arejee shuleni mara tu baada ya kumaliza mapumziko ya uzazi, ili aendelee na masomo yake kama inavyoelekezwa na sera ya elimu jumuishi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uyui ambaye pia anakaimu Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Mohamed Mtulyakwaku, alimshukuru Mhe. Chacha kwa kuchukua hatua stahiki na kuwaasa walimu kuzingatia wito wao na kufanya kazi njema waliyoitiwa na Mwenyezi Mungu ya kuelimisha dunia kwa upendo na bidii.
Ziara hii imeacha ujumbe mzito kwa viongozi wa shule, jamii na serikali kwa ujumla kuhusu umuhimu wa malezi ya watoto wa kike, ufuatiliaji wa karibu wa maendeleo yao, na uwajibikaji usioyumba kutoka kwa walimu na watumishi wa umma.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa