Katika hatua ya kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paulo Chacha, ameongoza oparesheni maalum ya kuteketeza mashamba ya bangi yaliyogundulika ndani ya hifadhi ya mto Igombe, iliyopo katika Manispaa ya Tabora.
Oparesheni hiyo, ambayo imesheheni ushirikiano kati ya viongozi wa serikali, jeshi la polisi,jeshi la akiba na mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya, imelenga kusafisha eneo hilo na kufikisha ujumbe mkali kwa wale wote wanaojihusisha na kilimo haramu cha bangi.
Akizungumza mara baada ya zoezi hilo, Mhe. Chacha alielezea kwa ukali kutoridhishwa na tabia ya baadhi ya wananchi wanaovamia maeneo ya hifadhi na kuendesha shughuli haramu za kilimo cha bangi.
“Bangi ni zao haramu ambalo linaangamiza vijana wetu na kuharibu nguvu kazi ya taifa. Serikali na jamii kwa ujumla hatuwezi kulikubali hili. Natoa onyo kali kwa wote wanaojihusisha na kilimo hiki waache mara moja,” alisisitiza Mhe. Chacha, akiongeza kuwa kuishi hifadhini na kulima bangi ni makosa mawili makubwa ya kisheria.
Katika oparesheni hiyo, Jeshi la Polisi mkoani Tabora limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 11 – wanaume 9 na wanawake 2 – waliokutwa wakiendesha shughuli za kilimo cha bangi katika eneo hilo. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Richard Abwao, alieleza kuwa tayari wamekamata magunia 25 ya bangi katika oparesheni hiyo.
“Tutahakikisha wauzaji wakubwa wa bangi wanakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Huu ni mwanzo wa oparesheni endelevu,” alisema Kamanda Abwao. Alitoa rai kwa wananchi kuachana na kilimo haramu na kuhamasisha shughuli halali za kiuchumi.
Kwa upande wake, Afisa Oparesheni kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini, Ndg. Godfrey Renatus, ameeleza kuwa zaidi ya ekari tano za mashamba ya bangi zimeteketezwa katika oparesheni hiyo. Alisisitiza kuwa sheria itachukua mkondo wake kwa wote wanaobainika kujihusisha na biashara hiyo haramu.
“Tunaomba wananchi washirikiane nasi kwa kutoa taarifa kupitia namba 119. Usiri wa taarifa zao utahakikishwa kikamilifu,” alisema Ndg. Renatus.
Mapambano dhidi ya dawa za kulevya yameendelea kuwa kipaumbele kwa serikali na mamlaka zake, huku wito ukiendelea kutolewa kwa jamii kushiriki kikamilifu kuokoa kizazi kijacho kutokana na madhara ya matumizi na biashara ya dawa hizo haramu.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa