Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paulo Chacha, ameonesha masikitiko makubwa na ghadhabu kufuatia vitendo vya udanganyifu vinavyofanywa na baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi vya wakulima wa pamba (AMCOS) katika Wilaya ya Igunga.
Hatua hiyo imekuja baada ya timu maalum kutoka Wizara ya Kilimo kutoa taarifa ya ukaguzi wa mizani za kielektroniki zinazotumika kupima zao la pamba, ambapo walibaini kuwepo kwa mchezo mchafu wa kuchakachua mizani na kusababisha wizi mkubwa wa zao hilo.
Katika taarifa hiyo, imeelezwa kuwa mizani 107 ilisambazwa na Serikali kwa vyama vya msingi katika Wilaya ya Igunga, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha wakulima wanapata haki yao kwa kupimiwa pamba kwa usahihi, baada ya kuwepo malalamiko ya awali kuhusu mizani za kizamani.
Hata hivyo, uchunguzi umebaini kuwa vyama 32 vya msingi vimehusika na hujuma ya kuchakachua mizani hizo mpya, na kusababisha upotevu wa zaidi ya kilo 998,977 za pamba zenye thamani ya shilingi milioni 596.38 katika msimu huu pekee wa ununuzi.
Mheshimiwa Chacha amesema vitendo hivyo ni uhujumu wa uchumi vinavyolenga kuwakandamiza wakulima wa kawaida wanaojituma kuzalisha, na kwamba Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitavumilia kabisa aina hiyo ya uonevu na
wizi.
Amezitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali, za haraka na kisheria kwa wote waliohusika, akisisitiza kuwa mkoa wa Tabora hautakuwa mahali salama kwa watu wanaotumia nafasi zao kuwadhulumu wananchi.
Tayari taarifa ya uchunguzi imewasilishwa kwa vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi, huku serikali ikiahidi kuimarisha mifumo ya usimamizi wa ununuzi wa mazao kuhakikisha wakulima wananufaika na jasho lao.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa