Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, ameongoza kikao cha utengaji wa maeneo kwa ajili ya utekelezaji wa programu ya BBT Kilimo. Kikao hicho kilihudhuriwa na kamati ya usalama ya mkoa, wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya, wakurugenzi watendaji, pamoja na wakuu wa divisheni na vitengo. Kikao hicho kilifanyika katika ukumbi mdogo wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Akifungua kikao hicho Mhe. Chacha amesema anatumaini kupitia kikao hicho kitawajengea uelewa wa pamoja wataalam pamoja na viongozi wa mkoa wa Tabora ili sasa waweze kwenda kutekeleza mpango huo kwa ufanisi utakaoleta matokeo makubwa mkoani Tabora.
Katika mada ya utengaji wa maeneo, Bw. Samson Poneja, Mkurugenzi Msaidizi - Sehemu ya Pembejeo za Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, alisisitiza kuwa mpango wa BBT Kilimo utakuwa suluhisho muhimu katika kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha kutosha. Aidha, aliongeza kuwa mpango huu utaongeza ajira za moja kwa moja kwa vijana na kwa watu wengine watakaoshiriki katika shughuli za kilimo.
Kwa upande mwingine, Ndg. Yobu Kiungo, Bwana Miti mkuu mkoa wa Tabora, alitoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuchangamkia fursa ya biashara ya hewa ya kaboni. Alieleza kuwa mkoa wa Tabora una maeneo yanayofaa kwa ajili ya uwekezaji katika biashara hii ya kimkakati, na kwamba itatoa faida kubwa kutokana na ufanisi na uhakika wa kipato kama jinsi unavyoonekana katika maeneo mengi nchini.
Wataalam na viongozi walikubaliana kwa pamoja na mpango huo, na walieleza ahadi yao ya kuutekeleza katika maeneo yao kwa kuzingatia sheria na maelekezo yaliyotolewa katika kikao hicho.
Akifunga kikao hicho kwa niaba ya Mhe. Chacha, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua, Dkt. Gelard Mongella, alisisitiza kuwa kila wilaya katika mkoa wa Tabora inapaswa kutenga eneo lisilopungua ekari 5000 na kuendelea, kwa ajili ya utekelezaji wa mpango wa BBT Kilimo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa