Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha amepokea rasmi ujumbe wa wageni kutoka Shirika la A Light to the Nations (ALN) lenye makao yake makuu nchini Marekani, waliowasili ofisini kwake kwa lengo la kujitambulisha na kueleza dhima ya ziara yao mkoani humo.
Ujumbe huo umeongozwa na mwenyeji wao, Mchungaji Rashid Hassan wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania – Kidatu, na unajumuisha Mchungaji Joseph Kalyango kutoka Uganda pamoja na Mchungaji Isaack Maliyamungu kutoka Rwanda.
Katika ziara yao mkoani Tabora, ujumbe huo unatarajia kutembelea shule za msingi na sekondari katika wilaya za Tabora Manispaa,Urambo, Kaliua, Sikonge, Uyui na Nzega, ambako watapata fursa ya kuzungumza na wanafunzi pamoja na vijana kuhusu masuala ya maadili na malezi bora.
Lengo kuu la ziara hiyo ni kutoa elimu kwa vijana kuhusu hatari za matumizi ya dawa za kulevya, kuwahamasisha kuishi kwa kufuata maadili mema, pamoja na kuwajengea mtazamo chanya wa maisha unaozingatia misingi ya nidhamu, uwajibikaji na heshima katika jamii.
Sambamba na shughuli hizo za uhamasishaji, ujumbe huo pia unatarajia kutoa msaada wa vifaa vya michezo, hususan mipira ya mpira wa miguu na pete, kwa baadhi ya shule zitakazotembelewa, kama sehemu ya kuunga mkono maendeleo ya michezo na kukuza afya na mshikamano miongoni mwa vijana wa mkoa wa Tabora.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa