Mkoa wa Tabora umeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya mawasiliano baada ya utekelezaji wa Mradi wa Tanzania ya Kidijitali (DTP) unaosimamiwa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ambapo minara 50 ya mawasiliano ya simu na intaneti imejengwa kwa lengo la kuondoa maeneo yasiyo na mawasiliano na kupanua upatikanaji wa huduma hizo vijijini na pembezoni.
Kabla ya mradi huu, vijiji vingi mkoani Tabora vilikosa kabisa mtandao wa simu na intaneti, hali iliyowalazimu wananchi kusafiri umbali mrefu kupata huduma za msingi za mawasiliano, kifedha na taarifa. Baada ya utekelezaji wa mradi, vijiji 99 sasa vimeunganishwa na mawasiliano, hatua iliyoboresha kwa kiasi kikubwa maisha ya wananchi na shughuli zao za kiuchumi na kijamii.
Kwa mujibu wa takwimu za utekelezaji, mradi umehusisha wilaya zote saba za mkoa wa Tabora, kata 45 na vijiji 99, ambapo minara yote 50 iliyopangwa imekamilika kwa asilimia 100 na kuanza kutoa huduma, na kufanya Tabora kuwa miongoni mwa mikoa iliyopata idadi kubwa ya minara ya mawasiliano nchini.
Huduma hizo sasa zimefika hata katika maeneo magumu kufikika yakiwemo ya porini, yaliyo mbali na barabara kuu na pembezoni kabisa kama Ipole, Usunga na Ugunga, hali iliyoleta mafanikio ya kimkakati katika kufungua maeneo hayo kijiografia na kiuchumi.
Minara hiyo inahudumiwa na makampuni mbalimbali ya simu yakiwemo Airtel, Vodacom,Halotel,TTCL pamoja na Yas, hatua iliyoongeza ushindani wa huduma, kuboresha ubora wa mtandao na kupunguza gharama za mawasiliano kwa wananchi wa mkoa wa Tabora.
Kwa ujumla, utekelezaji wa mradi huu umeleta athari chanya ikiwemo kuongezeka kwa mawasiliano ya simu na intaneti vijijini, kuimarika kwa elimu kwa njia ya TEHAMA, kuboreshwa kwa huduma za afya kwa mifumo ya kidijitali, kukua kwa biashara, kilimo na ujasiriamali wa kidijitali pamoja na kurahisisha upatikanaji wa huduma za serikali mtandao.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa