Akimwakilisha Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Kaimu Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Ndg. Dietrich Mwinuka, ameongoza kikao cha utambulisho wa Mradi wa YEFFA (Youth Entrepreneurship for the Future of Food and Agriculture) unaotekelezwa kwa ushirikiano kati ya Tanzania Agricultural Modernization Association (TAMA) na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), kilichofanyika katika ukumbi mdogo wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.
Awali akiwasilisha maelezo ya mradi huo, Afisa Ufuatiliaji na Tathmini kutoka TAMA, Ndg. Frank Shinge, amesema kuwa mradi wa YEFFA unalenga kuwajengea uwezo vijana kupitia mafunzo ya ufundi stadi katika maeneo ya uendeshaji na matengenezo ya mitambo ya kilimo (agro-mechanization), mifumo ya umwagiliaji pamoja na usindikaji wa mazao. Ameongeza kuwa mradi huo unafadhiliwa na Shirika la AGRA, na utekelezaji wake umeanza rasmi mwezi Novemba 2025 na unatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba 2027.
Ndg. Shinge amesema kuwa mradi huo unatekelezwa katika mikoa minne ya Kanda ya Kati ambayo ni Tabora, Manyara, Singida na Dodoma, na unatarajia kuwawezesha jumla ya vijana 1,525 kwa kuwapatia mafunzo ya moja kwa moja katika ujuzi wa umechanishaji wa kilimo, ikiwemo uendeshaji na matengenezo ya mitambo ya kilimo, umwagiliaji pamoja na usindikaji wa mazao.
Ameeleza kuwa, katika utekelezaji wake, mradi wa YEFFA umeweka mkazo mkubwa katika usawa wa kijinsia ambapo asilimia 70 ya wanufaika wanatarajiwa kuwa wanawake, kwa lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika kilimo cha kisasa chenye tija na mchango mkubwa katika uchumi wa familia na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wao, washiriki wa kikao hicho waliotoka katika taasisi za kidini, wawakilishi wa makundi maalum pamoja na asasi za kiraia, wameupokea mradi huo kwa moyo wa shukrani na kuahidi kuwa mabalozi wema wa kuhamasisha vijana kuomba kujiunga na mafunzo hayo ya muda mfupi yenye tija kubwa katika kujiajiri na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mtu binafsi na taifa.
Kwa mujibu wa taratibu za mradi, sifa za kujiunga na mpango huo ni kwa raia wa Tanzania kutoka mikoa husika, wenye umri kati ya miaka 18 hadi 35 na wenye elimu kuanzia darasa la saba na kuendelea. Fomu za maombi zinapatikana kupitia tovuti ya Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) pamoja na katika ofisi za VETA za mikoa husika.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa