Na. OMM Tabora.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma, Mhe. Augustine Vuma Holle, Mbunge wa Kasulu Vijijini, leo ameiongoza kamati hiyo kukagua ujenzi wa jengo la makao makuu ya Bodi ya Tumbaku Kanda ya Magharibi, mkoani Tabora.
Jengo hilo, ambalo linajengwa kwa gharama ya shilingi bilioni 1.2, linatekelezwa na mkandarasi Suma JKT na kusimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA). Hadi sasa, ujenzi umefikia asilimia 93 ya utekelezaji.
Katika ziara hiyo, Mhe. Vuma alikiri juhudi nzuri za Bodi ya Tumbaku katika kuwasimamia wakulima wa tumbaku nchini, akiwatia moyo kuendelea kuboresha uzalishaji wa tumbaku kwa manufaa ya wakulima. “Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya. Endeleeni kuchapa kazi na kuimarisha sekta hii kwa faida ya wakulima na uchumi wa nchi yetu,” alisema Mhe. Vuma.
Vilevile, Mhe. Vuma alitoa pongezi kwa Suma JKT na TBA kwa utekelezaji wa mradi huo, akisisitiza kwamba thamani ya fedha inaonekana wazi katika hatua zilizofikiwa. Wajumbe wa kamati hiyo walishauri kuwa jengo hilo likamilike kwa wakati ili liweze kutoa huduma kwa wananchi na pia kuwa chanzo cha mapato kwa serikali.
Katika maelekezo yake, Mhe. Vuma alisisitiza umuhimu wa mkandarasi kusimamiwa vyema ili ujenzi ukamilike kwa wakati. Aliagiza TBA kuchukua hatua za kuhakikisha jengo hilo linatunzwa vizuri kwa manufaa ya umma na kudumu kwa muda mrefu, ili kuleta faida endelevu kwa serikali.
Ziara hiyo imeonyesha mafanikio ya utekelezaji wa mradi huo na imesisitiza dhamira ya serikali katika kuboresha miundombinu ya uchumi wa kisasa na kuendeleza sekta ya tumbaku nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa