Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Paulo Chacha, ameshiriki dua maalum ya kuliombea taifa kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025. Dua hiyo imeandaliwa na Kamati ya Amani ya Mkoa wa Tabora na kufanyika katika uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui, ikihudhuriwa na waumini wa dini na madhehebu mbalimbali.
Akitoa salamu kwa niaba ya Kamati ya Amani ya Mkoa wa Tabora, Sheikh wa Mkoa wa Tabora, Ibrahimu Mavumbi, alisema lengo kuu la kusanyiko hilo ni kuonesha uzalendo na kuenzi amani na utulivu wa nchi.
“Uislamu unatambua kwamba uzalendo wa mwanadamu kuipenda nchi ni wajibu wake, pale ambapo kiongozi wetu mkubwa Mtume Mohamed (SAW) aliposema kwamba hakika alama ya Imani ya muislamu/muumini ni kuipenda nchi yake,” alisema Sheikh Mavumbi na kusisitiza kuwa ni jukumu la kila mmoja kuitetea na kuilinda amani ya taifa.
Kwa upande wake, Baba Askofu Muadhama Kardinali Protase Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Tabora, aliishukuru Kamati ya Amani kwa kuwakutanisha watu wa dini na madhehebu mbalimbali kwa nia njema ya kuombea amani na utulivu wa taifa.
“Ndugu zangu, tuombee amani lakini tulifanye hilo sote kwa pamoja, tukishirikiana kwa pamoja bila unafiki, bila kujifanya kwa sababu muonekane hivi, na hakika kabisa tunaweza tukalipata na nchi yetu ikaendelea na tukawa bora katika amani hiyo ambayo tunaitafuta,” alifafanua Kardinali Rugambwa.
Akihutubia wananchi waliojitokeza kwa wingi kushiriki dua hiyo, Mheshimiwa Chacha aliipongeza Kamati ya Amani kwa uratibu mzuri wa tukio hilo na kuwahakikishia wananchi kuwa usalama upo wa kutosha kuelekea uchaguzi mkuu.
“Niwahakikishieni na niwape uhakika, amani ipo ya kutosha, laleni usingizi, fanyeni shughuli zenu kwa uhuru. Siku ya tarehe 29, ninyi nyote jitokezeni mkachague viongozi mnaowataka kuwaongozeni, bila hofu wala kuogopa. Hakuna mtu anayeweza kukudhuru, serikali ipo kwa ajili yenu,” alieleza Mheshimiwa Chacha.
Tukio hilo limebeba ujumbe wa mshikamano, upendo na uzalendo, likisisitiza dhamira ya mkoa wa Tabora kuendelea kuwa mfano wa amani, utulivu na umoja wa kitaifa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa