Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amekabidhi jumla ya kompyuta 8 kwa Jeshi la Magereza mkoani humo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha mfumo wa “Kesi Mtandao” unaolenga kurahisisha usikilizaji wa mashauri ya mahabusu na wafungwa bila usumbufu wa kusafiri mahakamani. Tukio hilo limefanyika leo katika Gereza Kuu la Uyui, mkoani Tabora.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Jaji Dkt. Adam Juma Mambi, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora, alisema Mahakama inaendelea kutekeleza mkakati wa matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa haki kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya taifa. Alibainisha kuwa upatikanaji wa vifaa hivyo utasaidia kuongeza ufanisi katika usikilizaji wa mashauri bila wafungwa kuhudhuria moja kwa moja mahakamani.
“Kwa mwaka 2024/25 jumla ya mashauri 421 yamesikilizwa kwa njia ya mtandao, jambo ambalo limepunguza safari zisizo za lazima za kusafirisha wafungwa na watuhumiwa kwenda mahakamani, na hivyo kuongeza kasi ya utoaji haki kwa haraka na kwa wakati,” alisema Jaji Dkt. Mambi.
Katika hotuba yake baada ya kukabidhi vifaa hivyo pamoja na magodoro 168 kwa ajili ya wafungwa wa Gereza Kuu la Uyui, Mhe. Chacha aliwahimiza viongozi wa Mahakama na Magereza kutoshindwa kutekeleza majukumu yao kutokana na changamoto zinazoweza kuzuilika.
“Mhe. Jaji, sisi kama Serikali tupo bega kwa bega na vyombo vya utoaji haki. Usikumbane na changamoto yoyote ukakaa kimya. Ikiwa kuna jambo linalohitaji ushirikiano wa Serikali, nijulishe mapema ili tutatue changamoto hizo na kuruhusu kazi zenu ziendelee kwa ufanisi,” alisisitiza Mhe. Chacha.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Gereza Kuu la Uyui, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Musa Mkisi, aliishukuru Serikali kwa msaada wa vifaa vya TEHAMA na magodoro, akisema vitachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza mlundikano wa kesi na kuimarisha mazingira ya wafungwa.
Utekelezaji wa mfumo wa Kesi Mtandao mkoani Tabora unaendelea kuwa mfano bora wa matumizi ya teknolojia katika utoaji wa haki, sambamba na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha mifumo ya kidijitali katika taasisi za umma, kwa lengo la kuongeza uwazi, ufanisi, na upatikanaji wa haki kwa wakati.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa