Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kupokea maji kutoka Ziwa Viktoria na kusambaza katika miji ya Tabora, Igunga na Nzega unaotekelezwa na Wizara ya Maji.Kauli hiyo imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mheshimiwa Japhet Hasunga (Mb) wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo na baadae kupokea taarita ya utekelezaji wa mradi huo kwa awamu ya Kwanza na ya pili.
Kamati inaipongeza TUWASA kwa kusimamia vizuri mradi huo na kufikia malengo ya Serikali ya kufikisha maji safi na salama kwa wananchi katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa ukame ambayo hayana vyanzo vya maji vya uhakika.
Sambamba na hilo, Mheshimiwa Hasunga amewasisitiza TUWASA kuhakikisha wanaongeza umakini na usimamizi wa miundombinu ya mradi huo kwa lengo la kuondoa kabisa changamoto ya upotevu wa maji ili wananchi wengi zaidi waweze kunufaika na mradi huo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Tabora (TUWASA) Mhandisi Mayunga Kashilimu amesema kukamilika kwa mradi huo kumewezesha wananchi zaidi ya milioni moja na laki mbili (1,200,000) wanapata huduma ya maji safi na salama.
Aidha, Muhandisi Mayunga amesema kuwa, huduma bora ya Maji inachangia kuboresha afya za wananchi wa maeneo husika na kuinua uchumi kupitia maendeleo ya sekta zingine zinazotegemea maji kama vile viwanda. Kamati ya PAC, kesho inatarajia kukagua mradi wa kiwanda cha kupaka rangi mabomba kwa ajili ya kuweka mfumo wa upashaji joto mabomba katika mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa