Na. OMM Tabora.
Serikali kupitia Wizara ya Afya imejipanga kuhakikisha kuwa hospitali zote na vituo vyote vya afya nchini vinakuwa na kliniki za kutolea huduma kwa wagonjwa wa siko seli (seli mundu), ili kuwafikia wagonjwa wengi zaidi kwa wakati.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Benedict Komba, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Siko Seli Duniani yaliyofanyika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete. Dkt. Benedict amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha mazingira rafiki ya utoaji wa huduma, na ametoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali kwa kuwapeleka watoto hospitalini mara tu wanapobainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete, Dkt. Joachim Eyembe, amesema hospitali hiyo imeweka utaratibu wa kuwapima watoto wachanga ili kubaini mapema ugonjwa huo. Amesisitiza kuwa huduma za kliniki kwa wagonjwa zitaendelea kutolewa pamoja na ushauri nasaha kwa familia na jamii kwa ujumla.
Takwimu zinaonesha kuwa hadi sasa, Tanzania ina zaidi ya wagonjwa wa siko seli 14,000 waliogunduliwa, ambapo zaidi ya wagonjwa 8,000 wanatokea mkoani Tabora pekee. Ugonjwa huu wa kurithi kutoka kwa wazazi kwenda kwa watoto unaendelea kuwa changamoto inayohitaji hatua za haraka na madhubuti.
Maadhimisho ya Siku ya Siko Seli huadhimishwa kila mwaka ifikapo Juni 19, na kwa mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo: "Hatua Madhubuti za Kitaifa kwa Matokeo Chanya ya Kijamii; Kuwezesha Jamii Kutambua, Kuzuia na Kukabiliana na Siko Seli."
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa