Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imezindua rasmi utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Scheme ya Umwagiliaji ya Mwamapuli iliyopo Kijiji cha Mwanzugi katika Kata ya Igunga, Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora. Mradi huu unalenga kuongeza eneo la umwagiliaji kutoka hekta 630 hadi kufikia hekta 2,397, sawa na ekari 5,923, ambapo wakulima zaidi ya 2,470 wanatarajiwa kunufaika moja kwa moja na mradi huo.
Akisoma taarifa ya mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji wa Mkoa wa Tabora,Francis Mgangaluwa, alisema kuwa mradi huu unakusudia kuongeza tija katika kilimo cha umwagiliaji kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa mazao na kipato kwa wakulima wa eneo hilo. Aidha, mradi huu utasaidia kuongeza usalama wa chakula katika Mkoa wa Tabora na nchi kwa ujumla.
Utekelezaji wa mradi huu utafanywa na Mkandarasi mzawa, kampuni ya Salum Motors Transport (SAMOTA) kutoka Nzega, chini ya usimamizi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji. Mkataba wa ujenzi ulisainiwa tarehe 7 Machi 2025, na kazi zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 10 Juni 2025. Mradi huu utatekelezwa kwa kipindi cha siku 720, ambapo thamani yake ni shilingi bilioni 26.9.
Kazi zitakazofanyika katika mradi huu ni pamoja na ujenzi wa barabara za mashambani zenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha changarawe, ujenzi wa mifereji ya matupio yenye urefu wa kilomita 27, pamoja na ujenzi wa mitalo ya zenge, vigawa maji, box karavati saba na pipe karavati. Pia kutajengwa ofisi ya Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, nyumba ya Meneja wa Scheme pamoja na ununuzi wa gari moja kwa ajili ya usimamizi wa mradi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, aliwapongeza wakulima wa Igunga kwa ushirikiano wao mkubwa kwa Tume ya Umwagiliaji na uongozi wa Wilaya ya Igunga katika maandalizi ya mradi huu. Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa fedha kiasi cha shilingi bilioni 26 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo muhimu wa maendeleo. Dkt. Mboya alitoa wito kwa Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi kwa ubora wa hali ya juu na kwa wakati uliopangwa, akisisitiza kuwa viongozi wa mkoa watakuwa karibu katika kusimamia kila hatua ya utekelezaji.
Katika hatua nyingine, Dkt. Mboya alionesha kusikitishwa na mila na desturi zinazokwamisha maendeleo ya wananchi wa kijiji cha Chumachankola, waliopinga utekelezaji wa mradi kwa madai kuwa eneo hilo hutumika kwa ajili ya matambiko. Alitoa wito kwa wananchi kubadilika kifikra na kuendana na maendeleo ya karne ya sayansi na teknolojia, akisema ni wakati wa kuachana na mila zinazokwamisha juhudi za Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, Mhe. Sauda Mtondoo, alieleza kuwa mradi huo ni uti wa mgongo wa uchumi wa wananchi wa Igunga, kwani unaleta uhakika wa uzalishaji wa chakula bila kutegemea mvua. Alisisitiza kuwa Serikali ya awamu ya sita imedhamiria kwa dhati kuinua uchumi wa wananchi kupitia uwekezaji mkubwa katika sekta ya umwagiliaji.
Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, akihutubia wananchi waliohudhuria hafla ya kukabidhi rasmi mradi huo kwa Mkandarasi, aliwashukuru wananchi wa Igunga kwa kuupokea mradi kwa moyo wa uzalendo na ushirikiano. Hata hivyo, alilaani vikali kitendo cha baadhi ya wananchi wa kijiji cha Chumachankola kupinga mradi kwa sababu ya kulinda eneo la matambiko. Aliahidi kuwa Serikali ya Mkoa italifanyia kazi suala hilo kwa busara na hekima ili kupata suluhu ya kudumu. Mhe. Chacha pia aliwakumbusha wanachama wa scheme hiyo kuhakikisha wanalipa ada zao kwa wakati na kwa uaminifu, huku akisisitiza umuhimu wa viongozi wa scheme kuwa na uwazi katika usomaji wa mapato na matumizi kwa wanachama wao.
Katika hatua nyingine ya hotuba yake, Mhe. Chacha alikemea vikali kitendo cha raia mmoja kuchana kitambulisho cha Afisa wa TAKUKURU aliyekwenda kutekeleza wajibu wake kwa mtuhumiwa, akisema kuwa Serikali haitavumilia tabia ya wananchi kuchukua sheria mkononi au kupambana na watumishi wa umma walioko kazini. Alitoa onyo kali kwa yeyote atakayejaribu kuzuia au kuvuruga utekelezaji wa sheria za nchi.
Viongozi wa Wilaya ya Igunga kwa pamoja waliahidi kushirikiana kikamilifu kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa wakati, kwa ubora na unatunzwa ipasavyo kwa manufaa ya wananchi wote wa Igunga na Mkoa wa Tabora kwa ujumla.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa