Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameongoza maadhimisho ya Siku ya Wauguzi Duniani yaliyofanyika kimkoa katika ukumbi wa mikutano wa Chief Isike Mwanakiyungi mjini Tabora. Maadhimisho haya yamefanyika leo tarehe 30 Mei, yakibeba kaulimbiu isemayo “Uuguzi Ni Nguvu ya Mabadiliko Duniani”, yakilenga kutambua mchango wa wauguzi katika maendeleo ya sekta ya afya duniani.
Akisoma risala kwa niaba ya wauguzi wa Mkoa wa Tabora, Katibu wa Chama cha Wauguzi Tanzania (TANNA) mkoani wa Tabora, Frank Haule, alieleza kuwa wauguzi wamekuwa sehemu muhimu ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya nchini. Alisema kuwa mchango wao hauwezi kupuuzwa na kwamba kazi wanayoifanya ni ya kipekee na ya kujitolea kwa kiwango cha juu. Haule aliishukuru serikali kwa kukubali kubadilisha muundo wa utumishi wa kada ya Uuguzi, hatua ambayo amesema italeta tija na kuwapa hamasa wauguzi kote nchini.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kuiomba serikali kuendelea kuajiri watumishi wa kada ya uuguzi ili kukidhi mahitaji ya wananchi, pamoja na kujengewa uwezo vituoni ili kuendana na mabadiliko ya kisasa, hususan mafunzo ya huduma kwa wateja. Alisisitiza umuhimu wa wauguzi kulipwa posho zao stahiki kama vile posho za mazingira hatarishi, posho za kuitwa kazini, posho za masaa ya ziada, na posho za sare za kazi, ili kuongeza ari ya utendaji kazini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, Ndg. Elihuruma Nyella, aliwapongeza wauguzi kwa kazi kubwa wanayoifanya katika jamii na kueleza kuwa serikali inaendelea na zoezi la kuajiri watumishi wapya wa umma. Alisema kipaumbele kimewekwa katika kada ya afya, hasa upande wa uuguzi kwa kuwa ni kada muhimu katika ustawi wa huduma za afya nchini.
Naye Katibu Tawala Msaidizi anayeshughulikia Afya, Dkt. Honoratha Rutanisibwa, aliwaunga mkono viongozi wenzake kwa kuwapongeza wauguzi kwa moyo wa kujituma katika kazi yao. Aliwahimiza wauguzi hao kuendelea kutoa huduma bora kwa wananchi kwa staha na utu, huku akisisitiza kuepuka matumizi ya lugha chafu kwa wagonjwa, ulevi kazini, na mavazi yasiyofaa kwa baadhi ya wauguzi wachache. Alisema kuwa serikali imewekeza fedha nyingi katika kuboresha miundombinu ya afya na hivyo ni wajibu wa wauguzi kuhakikisha wananchi wananufaika na huduma bora.
Akihitimisha maadhimisho hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, aliwapongeza wauguzi wote wa mkoa wa Tabora kwa kujituma katika kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu. Alisisitiza umuhimu wa umahiri katika utoaji wa huduma za afya, hasa huduma za dharura, na kuagiza mkoa kupanga utaratibu wa kubaini maeneo yenye upungufu ili baadhi ya wauguzi wajengewe uwezo wa kitaalamu zaidi katika utoaji wa huduma hizo.
Akijibu risala ya wauguzi, Dkt. Mboya aliahidi kushughulikia haraka suala la kujengewa uwezo na kulipwa posho stahiki, na kuwaagiza waganga wakuu wa wilaya kulisimamia jambo hilo kwa uzito unaostahili.
Dkt. Mboya aliwakumbusha wauguzi kuendelea kufuata maadili na viapo vya wito wa huduma ya uuguzi, huku akionya kuwa wale watakaokiuka maadili hayo watachukuliwa hatua za kinidhamu. Aliagiza halmashauri zote kuendelea kuajiri wauguzi kwa mikataba ya muda wakati serikali ikiendelea kutenga bajeti ya ajira za kudumu. Pia alielekeza kuandaliwa mpango maalum wa upatikanaji wa chakula katika vituo vya kutolea huduma ili watumishi wa afya waweze kutekeleza majukumu yao kwa utulivu.Alisisitiza pia halmashauri zote kuhakikisha vituo vyote vya afya vinafungwa mfumo wa Gothmis hasa katika maeneo ambayo baddo hawajafanya hivyo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa