Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, ameongoza kikao kilichohusisha wataalamu wa afya ngazi ya mkoa na waandishi wa habari kuhusu tahadhari dhidi ya mlipuko wa ugonjwa wa mpox (monkeypox) nchini. Dkt. Mboya amewataka viongozi wa halmashauri zote kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu hatari ya ugonjwa huu na jinsi ya kujikinga.
Akitoa elimu ya kina kuhusu ugonjwa wa mpox, mratibu wa tiba wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Benedict Komba, alieleza kuwa ugonjwa huu ni wa mlipuko na unasababishwa na virusi ambavyo awali vilianzia kwa wanyama na kuhamia kwa binadamu. Dkt. Komba alisisitiza kuwa ugonjwa huu unaweza kuambukiza kupitia hewa, kugusa majimaji ya mwili wa binadamu aliyeambukizwa, au kugusa maeneo yaliyoathirika.
Dkt. Mboya alisisitiza kuwa elimu kuhusu tahadhari lazima iendelee kutolewa kwa wananchi, lakini pia wananchi wanatakiwa kuchukua hatua za kujikinga dhidi ya ugonjwa huu, kama walivyofanya wakati wa mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Aliwahimiza viongozi wa vijiji na vitongoji kutumia mifumo rasmi ya kiutawala ili kufikisha ujumbe wa tahadhari kwa wananchi.
"Ni muhimu wananchi watumie mifumo rasmi ya kiutawala ili kufikisha elimu ya tahadhari juu ya ugonjwa wa mpox. Ikiwa mgonjwa mwenye dalili za mpox atajitokeza, lazima apelekwe katika kituo cha afya ili apate matibabu sahihi. Waganga wa kienyeji wanatakiwa kuepuka kujihusisha na tiba za magonjwa ya mlipuko kwani zina hatari kwao na kwa wagonjwa," alisema Dkt. Mboya.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dkt. Honoratha Rutanisibwa, aliwatoa hofu wananchi, akisisitiza kuwa mkoa wa Tabora uko salama kwa sasa. Alieleza kuwa hakuna taarifa rasmi kutoka kwa wataalamu wa afya zinazothibitisha uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa mpox mkoani Tabora, lakini alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari.
Tahadhari hii inakuja wakati mkoa wa Tabora ukiwa ni moja ya mikoa inayopokea wageni wengi kutoka mikoa jirani ya Kigoma, Katavi, Singida, na Shinyanga, ambayo inapakana na nchi jirani za Congo, Rwanda, na Burundi. Hii inafanya muingiliano wa watu kuwa mkubwa, hasa kwa shughuli za kibiashara na usafirishaji. Hivyo, wataalamu wa afya wanasisitiza umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kuzuia kuenea kwa ugonjwa wa mpox.
Endelea kuchukua tahadhari ili kulinda afya yako na ya wengine.