Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Dkt. Khamisi Mkanachi, amemuwakilisha Mkuu wa mkoa wa Tabora,Mheshimiwa Paul Chacha katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake yaliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Nzega Mji, katika Uwanja wa Samora.
Akihutubia maelfu ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo, Mheshimiwa Mkanachi ameipongeza ofisi ya mkuu wa mkoa wa Tabora kwa usimamizi mzuri wa mikopo ya asilimia kumi, ambapo kati ya shilingi bilioni 3.9, wanawake wa mkoa wa Tabora wamewezeshwa shilingi bilioni 1.9 kupitia vikundi 226.
"Ndugu zangu, sisi katika Mkoa wa Tabora tumefanya jitihada mbalimbali kuhakikisha haki, usawa, na uwezeshaji wanawake unakwenda vizuri. Kuanzia Januari 2024 hadi Februari 2025, mikopo ya asilimia kumi yenye thamani ya shilingi bilioni 3.9 imetolewa, ambapo vikundi vinavyohusisha wanawake 226 vimepata fedha hizo. Wanawake pekee wamepokea bilioni 1.9, vijana bilioni 1.7, na walemavu milioni 264.3. Na katika suala la urejeshaji wa mikopo, kina mama ni wepesi, na wanarejesha kwa ufanisi mkubwa. Hii ni hatua nzuri katika kuwawezesha wanawake, nawapongeza sana," alieleza Dkt. Mkanachi.
Vilevile, Mheshimiwa Mkanachi alitoa rai kwa wanawake kuzingatia suala la malezi ya watoto, akisisitiza umuhimu wa kudumisha maadili mema na kuzungumza na watoto ili kutambua changamoto wanazokutana nazo. Aliongeza kuwa mmomonyoko wa maadili unazidi kuongezeka, na hivyo ni muhimu kuwa na muda wa kuwasikiliza watoto na kuhakikisha wanapata malezi bora.
Aidha, alisisitiza matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusema kuwa matumizi ya nishati mbadala ni bora na rahisi kuliko matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yanahatarisha mazingira. Alitoa wito kwa wananchi kuwa tayari kukubali mabadiliko haya, kwani dunia nzima inahama kwenye matumizi ya nishati zinazodhoofisha ustawi wa watu kwa kutumia nishati mbadala.
Mhe.Mkanachi pia alisisitiza umuhimu wa wananchi kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, akiwataka wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kufanikisha usawa na uwakilishi wa wanawake katika vyombo vya maamuzi.
Akitoa salamu kwa niaba ya wabunge wa Mkoa wa Tabora, Mheshimiwa Margaret Sitta, Mbunge wa Jimbo la Urambo, alisisitiza kuwa ili kufikia usawa ambao wanawake wanaupigania, ni muhimu kuzingatia suala la elimu. Alieleza kuwa bila maarifa, ni vigumu kufikia usawa wa kimaendeleo, hivyo ni jukumu la kila mwanamke kujiendeleza kielimu ili kusaidia mapambano ya ukombozi wa wanawake nchini.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa na Mhe. Mkanachi kwa kutoa vyeti vya pongezi kwa makundi mbalimbali ya wanawake mahili na wadau waliofanikisha shughuli muhimu ya maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa