Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa, amehitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora kwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi minne muhimu yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7. Miradi hii inatekelezwa katika Halmashauri ya Nzega Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Nzega, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali kuharakisha maendeleo katika mkoa wa Tabora.
Akitoa salamu za mkoa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Cornel Magembe, aliishukuru Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kuleta fedha nyingi za miradi ya maendeleo katika mkoa huo. Alisema kuwa fedha hizo zimeboresha huduma za elimu, afya, na miundombinu, na hivyo kurahisisha shughuli za uzalishaji na kuboresha maisha ya wananchi wa Tabora.
Wabunge wa jimbo la Bukene, Mhe. Selemani Zedi, na jimbo la Nzega Vijijini, Mhe. Hamisi Kigwangala, walieleza shukrani zao kwa serikali kwa kuleta fedha za miradi ya maendeleo. Walitaja mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na usimamizi mzuri wa miradi hiyo, ikiwemo kuboreshwa kwa huduma muhimu za kijamii na miundombinu katika wilaya ya Nzega na mkoa mzima wa Tabora.
Kwa upande wake, Mhe. Majaliwa aliwahakikishia wananchi wa Tabora kuwa serikali ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ipo imara na itaendelea kutekeleza miradi ya maendeleo kwa lengo la kuboresha maisha ya Watanzania. Alifurahishwa na kasi ya maendeleo iliyopatikana katika majimbo ya Nzega Mjini, Nzega Vijijini, na Bukene, akitaja kuwa ni matokeo ya usimamizi mzuri wa wabunge na ushirikiano kati ya Chama na Serikali katika mkoa wa Tabora.
Ziara ya Mhe. Majaliwa ilihitimishwa kwa kukagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi minne mikubwa ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na: Mradi wa ujenzi wa stendi ya mabasi katika Halmashauri ya Mji wa Nzega unaogharimu shilingi bilioni 4.2, Ujenzi wa shule ya amali ya Makomero yenye thamani ya shilingi bilioni 1.6, Ujenzi wa kituo cha afya Itobo chenye thamani ya shilingi milioni 500 pamoja na ujenzi wa shule mpya ya ufundi Mbagwa, ambapo mradi mzima unatarajiwa kugharimu shilingi bilioni 1.6.
Miradi hii ni uthibitisho wa dhamira ya serikali katika kuboresha sekta za elimu, afya, na miundombinu, na itaendelea kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya mkoa wa Tabora na nchi kwa ujumla.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa