Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ameongoza maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Tabora katika maadhimisho ya Wiki ya Chanjo Kitaifa yaliyofanyika katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Uyui. Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wakiwemo wananchi na wadau wa afya kutoka maeneo tofauti ya mkoa huo.
Katika maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Mhe. Deusdedith Katwale, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Mhe. Paul Chacha, alitoa pongezi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, kwa uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya uliosaidia kuboresha miundombinu na kuongeza upatikanaji wa dawa katika hospitali za mkoa huo.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, naye alitoa shukrani kwa serikali kwa uwekezaji wa zaidi ya shilingi bilioni 30.2 katika sekta ya afya. Alifafanua kuwa hadi kufikia Machi 2025, upatikanaji wa dawa mkoani Tabora umefikia asilimia 84. Aidha, aliwasisitiza watumishi wa afya kuendelea kuwajibika kwa kuzingatia maadili ya taaluma zao na kuwa mfano wa utoaji huduma bora kwa jamii.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) nchini Tanzania, Dkt. Charles Sagoe-Moses, aliwahimiza wazazi na walezi kushiriki kikamilifu katika kampeni za chanjo ili kusaidia kuokoa maisha ya wananchi. Alisisitiza umuhimu wa ushiriki wa jamii katika kuhakikisha chanjo zinawafikia walengwa wote kama njia ya kuimarisha afya ya umma.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, alibainisha kuwa mwaka huu wa maadhimisho ni wa kipekee kwani unatimiza miaka 50 tangu Tanzania ianze rasmi matumizi ya chanjo mbalimbali. Alieleza kuwa taifa linaendelea kuimarisha huduma za chanjo ili kupunguza vifo, kuzuia ulemavu na kulinda afya ya wananchi kwa ujumla.
Aidha, Waziri Mhagama alitaja magonjwa kama ndui, kifaduro na dondakoo kuwa miongoni mwa magonjwa yaliyotokomezwa kupitia kampeni za chanjo. Alitoa wito kwa wananchi kufuata ushauri wa wataalam wa afya, kubadili mitindo ya maisha, na kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko na magonjwa yasiyoambukiza. Maadhimisho haya yamebeba kaulimbiu isemayo: "Kinga ni Tiba: Tuungane Kuwezesha Walengwa Wote Wapate Chanjo."
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa