Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Matiko Chacha, ameonesha kuridhishwa na maendeleo ya miradi ya afya na elimu katika wilaya za Tabora na Nzega Mji, ambapo jumla ya shilingi bilioni 1.8 zimetumika kuboresha huduma katika sekta hizo muhimu.Hayo yamebainika leo katika ziara yake ya siku moja ya kukagua miradi ya maendeleo.
Miradi inayotekelezwa ni pamoja na ujenzi wa vituo vya afya na shule, ambapo ujenzi wa kituo cha afya Tumbi unaogharimu shilingi milioni 610.9, umefikia asilimia 89 ya utekelezaji ukihusisha ujenzi wa jengo la wagonjwa wa nje, maabara, jengo la mama na mtoto, pamoja na vyoo.Aidha,ujenzi wa kituo cha afya Itetemia unaojengwa kwa shilingi milioni 275.3, ambapo jengo la wagonjwa wa nje, maabara, na mifumo ya maji taka vimejumuishwa, na mradi huu umefikia asilimia 90.
Katika sekta ya elimu, mradi wa BOOST unaotekelezwa katika shule ya msingi Town kwa gharama ya shilingi milioni 318.8 ukihusisha ujenzi wa madarasa mawili ya kawaida, madarasa ya awali, matundu 20 ya vyoo, pamoja na ukarabati wa madarasa 17 na ofisi 5. Mradi huu umefikia asilimia 86. Vilevile, shule mpya ya sekondari Humbi katika halmashauri ya mji Nzega unaotekelezwa kwa shilingi milioni 603.8, ikiwa ni sehemu ya mradi wa SEQUIP. Ujenzi huu unajumuisha jengo la Tehama, maabara ya Fizikia, Kemia na Baiolojia, jengo la utawala, na madarasa manne na mradi umekamilika.
Akiongea na wananchi waliojitokeza katika ziara hiyo,Mhe. Chacha ametoa wito wkwa wananchi hao kuwahudumia kwa ukarimu wahudumu wa afya, ili wafaidi mazingira bora ya kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi. Aidha, alisisitiza kuwa mamlaka za serikali za mitaa zihakikishe vibarua wanaolipwa kwa kazi za ujenzi wanapata malipo yao kwa wakati.
Miradi hii, itakapokamilika, itaboresha huduma za afya na elimu katika maeneo ya pembezoni, ikiwemo huduma za uzazi na wagonjwa wa nje, na kutoa fursa bora za kujifunza kwa wanafunzi katika shule zilizozungukwa na changamoto za miundombinu. Hivyo, miradi hii ni hatua muhimu katika kuboresha ustawi wa jamii ya mkoa wa Tabora.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa