TABORA KWENDA KUNUFAIKA NA ZOEZI LA UPIMAJI NA UTAFITI WA AFYA YA UDONGO
Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Dkt. John Mboya, amewaaga wataalam wa udongo kutoka Wizara ya Kilimo waliokuwa mkoani humo kwa ajili ya zoezi la kitaifa la upimaji wa afya ya udongo, baada ya kukamilisha kazi ya awali ya uchukuaji sampuli na tathmini za kisayansi katika maeneo mbalimbali ya mkoa.
Wakitoa taarifa ya utekelezaji wa kazi hiyo, wataalam hao wamemueleza Dkt. Mboya kuwa zoezi la upimaji limefanyika kwa kufuata taratibu za kitaalamu na limehusisha maeneo ya ngazi ya kata na vijiji. Lengo la utafiti huo ni kupata takwimu sahihi zitakazowezesha kubaini hali halisi ya rutuba ya udongo na changamoto zinazokabili kilimo katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Tabora.
Wamefafanua kuwa baada ya uchambuzi wa maabara kukamilika, kila kijiji na eneo litapata taarifa kamili kuhusu aina ya udongo uliopo na namna bora ya kuutumia kwa shughuli za kilimo. Matokeo hayo yatawasaidia wakulima kupanga mazao yanayofaa, matumizi sahihi ya mbolea na mbinu bora za kuongeza uzalishaji, hatua itakayochochea kilimo chenye tija na endelevu.
Wataalam kutoka Wizara ya Kilimo waliofika kumuaga Katibu Tawala wa Mkoa ni pamoja na Bi. Sauda Mjape, Mratibu wa zoezi la upimaji wa afya ya udongo, akifuatana na Bw. Joseph Mbogoni, Mtaalam wa Udongo. Kwa upande wa uongozi wa mkoa, wageni hao waliongozwa na Ndugu Abrahaman Mndeme, Katibu Tawala Msaidizi Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, pamoja na Afisa Kilimo Bw. Mohamed Babu.
Akizungumza wakati wa kuwaaga wataalam hao, Dkt. Mboya aliwashukuru kwa kazi kubwa waliyoifanya na kueleza kuwa Serikali ya Mkoa wa Tabora ina matumaini makubwa na matokeo ya utafiti huo. Amesema utafiti wa afya ya udongo utaleta manufaa mapana kwa wananchi kwa kusaidia kupanga kilimo kinachozingatia ushahidi wa kisayansi na hivyo kuongeza tija kwa mkoa na Taifa kwa ujumla.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa