Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, amewaongoza viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika shughuli ya kuhani msiba wa Marehemu Mzee Nassoro Hamdan Seif, aliyekuwa mfanyabiashara maarufu na mmiliki wa mabasi ya NBS, pamoja na kiongozi mzalendo aliyejitoa kwa dhati katika kuhudumia jamii.
Viongozi wa kitaifa wa CCM waliohudhuria kutoa pole ni pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi na Mlezi wa Mkoa wa Tabora, Ndugu Nassr Ally, pamoja na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Ndugu Mohamed Said Mohamed.
Ugeni huo ulisindikizwa na viongozi mbalimbali wa chama na serikali, akiwemo Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Tabora, Ndugu Said Nkumba, Katibu wa CCM Mkoa, Komredi Wilson Khambaku, pamoja na viongozi wengine wa ngazi mbalimbali za mkoa.
Katika salamu zake za pole, Mhe. Chacha aliwasilisha rambirambi kutoka kwa Ndugu Suleiman Abubakar Mombo, mmoja wa viongozi wa kitaifa mwenye asili ya Mkoa wa Tabora, ambaye alishindwa kuhudhuria kutokana na majukumu mengine ya kitaifa.
Ujumbe huo wa viongozi ulipokelewa na Ndugu Mohamed Nassoro Hamdan, mtoto wa marehemu na Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Tabora, kwa niaba ya familia ya Marehemu Mzee Nassoro Hamdan Seif.
Akizungumza kwa niaba ya familia, Ndugu Mohamed Nassoro aliwashukuru kwa dhati viongozi wote wa chama na serikali kwa kufika kuwafariji na kushiriki katika maombolezo. Alieleza kuwa familia inathamini sana ushirikiano, faraja na mshikamano uliooneshwa tangu msiba ulipotokea hadi wakati wa mazishi.
Marehemu Mzee Nassoro Hamdan Seif anakumbukwa kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya usafirishaji na maendeleo ya jamii mkoani Tabora, ambapo ameacha alama ya uongozi, upendo na uzalendo kwa vizazi vijavyo.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa