Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mheshimiwa Paul Matiko Chacha amepokea madaktari Bingwa 40 ambao wamefika katika Mkoa wa Tabora kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa kwa Wananchi wa mkoa huu kupitia kambi ya siku tano, ambapo watakuwa katika hospitali za wilaya za halmashauri nane za hapa Tabora.
Akizungumza na Madaktari bingwa hao na baadhi ya viongozi wa wilaya za mkoa wa Tabora, Mhe Chacha amewaahidi madaktari hao uongozi wa mkoa na wilaya utahakikisha wanahamasisha wananchi ili wajitokeze kwa wingi katika hospitali za wilaya zao kupata huduma za madaktari hao.
“Kwasisi wananchi wa Mkoa wa Tabora hii ni fursa adhimu, tunatambua kabisa kuwa huduma mlizoletea ninyi wataalamu wetu wa afya zinaonyesha ni kwa kiasi gani Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana mapenzi mema na wananchi wa Mkoa huu” alisema Mhe Paul Matiko Chacha.
Na Katibu Tawala mkoa wa Tabora Daktari John Rogart Mboya, amesema Tabora kwa kipindi cha miaka mitatu huduma za Afya zimeimarika hasa katika upande wa miundombinu pamoja na wataalamu wa Afya mara baada ya kupokea Shilingi bilion 29.3.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ndugu Honoratha Rutatinisibwa ametoa taarifa ya madaktari waliopokelewa, amesema watakuwa katika Mkoa huu wa Tabora kwa siku tano kuanzia June 10 mpaka 14 mwaka 2024 na aliongeza kwa kusema kwa Madaktari hao 40 waliopokelewa, kila wilaya itapata madaktari watano wakiwemo wa Magonjwa ya wanawake, Magonjwa ya Watoto, usingizi, upasuaji na Magonjwa ya ndani.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa