Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Matiko Chacha, amezindua kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria, maarufu kama Mama Samia Legal Aid Campaign (MSLAC), katika uwanja wa Chipukizi, Manispaa ya Tabora. Uzinduzi huo umehudhuriwa na maelfu ya wananchi wa mkoa wa Tabora, ambao walijitokeza kushuhudia tukio hilo na pia kupata msaada wa kisheria kuhusu masuala mbalimbali, ikiwemo migogoro ya ardhi, mirathi, madai na masuala ya kijinai.
Akizungumza mbele ya umati huo, Mhe. Chacha ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Tabora kutumia fursa hii muhimu ya kupata msaada wa kisheria bure. Alisema, "Kampeni hii ina umuhimu wa kipekee katika kuongeza wigo wa ufikaji wa haki kwa wananchi, hasa wale walioko pembezoni na ambao hawawezi kumudu gharama za mawakili. Kampeni hii pia imekuwa msingi mzuri wa kujenga uelewa wa wananchi kuhusu haki zao za kikatiba na kisheria."
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Abdallah Sagini, ametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano mkubwa uliotolewa na mkoa, jambo ambalo lilisaidia kufanikisha uzinduzi wa kampeni hiyo. "Moja ya maeneo muhimu ambayo wizara inasimamia ni utoaji wa huduma ya msaada wa kisheria na uzingatiwaji wa haki za binadamu. Haya ni muhimu kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu kwani yanachangia moja kwa moja maendeleo ya taifa kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kufanya shughuli zao za kila siku pasipo hofu," alisema Mhe. Sagini.
Kampeni hii itatembelea halmashauri zote za mkoa wa Tabora na zaidi ya kata arobaini zitafikiwa kwa kipindi cha siku tisa, ikilenga kuwahudumia wananchi na kutatua changamoto mbalimbali za kisheria, hivyo kuimarisha utoaji wa haki nchini.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa