Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paul Chacha, ameongoza zoezi la makabidhiano ya magari mawili mapya kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa Jamii Salama, unaofadhiliwa na Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete. Zoezi hilo limefanyika nje ya ukumbi wa mikutano wa Isike Mwanakiyungi mkoani Tabora.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete, Bi. Vanessa Anyoti, alisema wilaya za Sikonge na Uyui zimechaguliwa kama sehemu za majaribio kwa ajili ya utoaji wa huduma za kliniki tembezi. Bi. Anyoti alieleza kuwa mradi huu utatoa uzoefu muhimu kwa wilaya na mikoa mingine nchini, na kuimarisha huduma za afya katika maeneo mengine.
Mradi wa Jamii Salama, unaotekelezwa katika wilaya hizi mbili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma za afya ya mama na mtoto nchini. Awamu ya kwanza ya mradi huu itahusisha utoaji wa huduma za kliniki tembezi,ujenzi wa zahanati mbili, Gengesita katika wilaya ya Uyui na Ipembe katika wilaya ya Sikonge, huku mkoa wa Tabora ukitumika kama mfano wa utekelezaji wa mradi huu.
Mhe. Chacha aliwataka viongozi wa wilaya hizi mbili kutumia magari hayo kwa malengo yaliyokusudiwa, akisisitiza kuwa ni muhimu kuhakikisha matumizi bora ya vifaa hivyo kwa kuvitunza na kuvifanyia ukarabati kwa wakati. Aidha, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Nkumba, alishukuru kwa kuanzishwa kwa mradi huo mkoani Tabora, akitaja kuwa huduma za afya zimeimarika sana, na mabadiliko ya utoaji huduma yameonekana wazi.
Kwa upande wao, wenyeviti wa Halmashauri za Sikonge na Uyui walitoa shukrani kwa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaletea mradi huo, wakisema utasaidia kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi wao.
Mbali na makabidhiano ya magari kwa ajili ya mradi wa Jamii Salama, Mhe. Chacha alikabidhi pia gari moja aina ya Isuzu kwa Katibu Tawala wa mkoa wa Tabora,Dkt. John Mboya, kwa ajili ya usambazaji wa chanjo katika mkoa wa Tabora. Aidha, alikabidhi magari matatu aina ya Ford kwa wakuu wa wilaya za Uyui, Nzega, na Urambo, ili kusaidia utoaji wa huduma bora za serikali katika maeneo yao.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa