Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tabora, Ndg. Said Juma Nkumba, amefungua kongamano la kilele cha maadhimisho ya miaka 48 ya kuzaliwa kwa chama hicho, lililofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tabora.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ndg. Nkumba ameupongeza umoja wa wazee mashuhuri wa historia na ushauri wa Tabora kwa kuandaa kongamano hilo kwa kushirikiana na uongozi wa CCM Mkoa wa Tabora na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora. Amesema mkoa wa Tabora umechukua nafasi muhimu katika historia ya harakati za kudai uhuru wa nchi yetu, huku akiwapongeza wataalam wa mkoa kwa juhudi zao katika kusimamia miradi ya maendeleo kwa ustadi mkubwa.
"Watumishi wetu wa serikali wanafanya kazi kubwa ya kusimamia fedha na rasilimali, ambazo kwa kweli zinatumika vyema na jamii inazidi kunufaika," alisema Ndg. Nkumba. "Endeleeni kufanya hivyo na sisi kazi yetu kubwa ni kuendelea kuwatia moyo ili muweze kuendelea kutekeleza majukumu yenu."
Katika kongamano hilo, Mzee Mohamed Said Salum, Mwandishi wa Vitabu na Mtaalamu wa Historia, alitoa mada kuhusu mchango wa mkoa wa Tabora katika historia ya ukombozi wa Tanganyika. Amesisitiza kuwa mkoa wa Tabora ni chimbuko la harakati za kudai uhuru na amewataka wananchi kupuuza propaganda za historia zilizopotoshwa, hasa kuhusu biashara ya watumwa. Amesema ni muhimu kujikita katika kuandika na kuhifadhi historia ya mashujaa wa hivi karibuni waliopigania uhuru.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, akimwakilisha Mkuu wa Mkoa, Dkt. John Rogath Mboya, amesema uchumi na maendeleo ya mkoa wa Tabora yanaendelea vizuri. Amebainisha kuwa pato la mkoa limeongezeka na kufikia shilingi trilioni 5.476, na wastani wa pato la mtu mmoja katika mkoa huo ni shilingi 1,850,000 kwa takwimu za mwaka 2024.
Dkt. Mboya ameongeza kuwa zaidi ya shilingi trilioni 1.1 zimepokelewa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, kilimo, mifugo, nishati, miundombinu na uwekezaji, na kuahidi kuwa serikali itaendelea kushughulikia masuala ya maendeleo kwa umakini mkubwa.
Alimaliza kwa kutoa wito kwa viongozi wa dini na wananchi wa mkoa wa Tabora kuwa mstari wa mbele katika kusimamia maadili mema na kupinga mambo yasiyofaa katika jamii, akisema kuwa serikali itaendelea kutekeleza wajibu wake kwa kuhakikisha maadili yanaenziwa katika jamii.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa