Mkuu wa Mkoa wa Tabora Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Burian amewataka wakazi wa mkoa wa Tabora na maeneo ya jirani kutunza miundombinu ya barabara ili fedha za serikali ambazo zimetumika kwenye uboreshwaji wa miundombinu hiyo kuwa na tija kwa taifa, ameyasema hayo leo Februari 21, 2024 alipofanya kikao na waandishi wa Habari katika ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Tabora.
Mhe. Batilda Burian amesema kuwa, kwa kipindi cha uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania uboreshwaji wa mindombinu ya barabara umefanyika kwa kiasi kikubwa sana na mpaka sasa mkoa wa Tabora umeunganishwa na mikoa mingine kwa barabara ya lami isipokuwa mkoa wa Mbeya unaounganishwa na barabara ya Ipole - Chunya ambayo tayari serikali imeshatenga fedha.
Mhe. Batilda amesema kuwa, uboreshwaji wa miundombinu ya barabara imekuza shughuli mbalimbali za kiuchumi zikiwemo, kilimo na biashara ambapo wananchi wameweza kusafirisha mazao na bidhaa mbalimbali ndani na nje ya mkoa wa Tabora na kukuza pato la taifa.
Ameongeza kuwa, wananchi wengi mkoani Tabora wamefaidika na utolewaji wa huduma za kijamii zikiwemo huduma za afya kutokana na uwepo wa miundombinu bora ya barabara.
Sambamba na hilo, Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa wito wa watendaji wa kata na vijiji kuhakikisha wanasimamia suala la utunzaji wa miundombinu ya barabara ambayo imekuwa ikiharibiwa mara kwa mara na wananchi wasio waadilifu hususani wizi na ufutwaji wa alama za barabara.
Aidha, RC Batilda ameupongeza uongozi wa TANROAD mkoa wa Tabora kwa jitihada za dhati katika kuhimarisha miundombinu ya barabara ambayo imekuwa na tija kwa mkoa na Tanzania kwa ujumla.
Tabora
S.L.P: 25 Tabora
Simu: 026 2604058
Mobile:
Barua Pepe: ras.tabora@tamisemi.go.tz
Haki Miliki ©2017 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Tabora .Haki zote zimehifadhiwa